Kaunti yasifu basari kwa kuboresha elimu

Kaunti yasifu basari kwa kuboresha elimu

Na SIAGO CECE

SERIKALI ya Kaunti ya Kwale imeahidi kutolegeza kamba katika utoaji basari kwa wanafunzi, kama njia mojawapo ya kuboresha viwango vya elimu katika eneo hilo

Gavana wa kaunti hiyo, Bw Salim Mvurya alisema kupitia kwa ufadhili wa karo, wanafunzi huondolewa wasiwasi kuhusu hatima ya elimu yao na hivyo kuwawezesha kupata matokeo bora masomoni.

Alisema Sh400 milioni zimetengwa kwa bajeti ya mwaka 2021 ili kuimarisha elimu hasa kwa wanafunzi wasiojiweza katika kaunti hiyo.

Alikuwa akiongea katika ukumbi wa Ukunda Social Hall mnamo Jumatano ambapo aliwapa wanafunzi 527 wa vyuo vikuu na shule za upili hundi za jumla ya Sh4.3 milioni katika wadi ya Ukunda.

Nazo Sh3.4 milioni ziliwaendea wanafunzi katika wadi ya Mackinnon.

“Tunafanya vyema, na hii ni kwa sababu, walimu, wanafunzi na wazazi pia hawana hofu yoyote,” Bw Mvurya alisema akiongeza kuwa kila wadi itapokea Sh20 milioni.

Alitoa mfano wa Shule ya Msingi ya Masimbani ambayo imekuwa kati ya shule bora zaidi Pwani kwa miaka mitatu mfululizo.

Katika eneobunge la Msambweni, zaidi ya wanafunzi 3,000 walipokea hundi za basari za Sh21 milioni kutoka kwa Mbunge wa Msambweni Feisal Bader kupitia Hazina ya Kitaifa ya Kustawisha Maeneobunge (NG-CDF).

“Tutaendelea kufanya miradi ambayo itaimarisha elimu eneo hili na pia, kuna nyingine kama vile kujenga na kurekebisha madarasa yaliyoharibika,” Bw Bader alieleza.

Katika eneobunge la Kinango, mbunge Benjamin Tayari alisema zaidi ya Sh9 milioni zimetolewa katika wadi saba huku wanafunzi 1,170 wa shule za sekondari wakipokea pesa hizo.

You can share this post!

Kaunti yatuma maafisa kuzima mzozo wa ardhi

Mswada unaolenga kudhibiti ulanguzi wa mihadarati...