Kaunti yatishia kushtaki Wizara ya Utalii kwa Rais

Kaunti yatishia kushtaki Wizara ya Utalii kwa Rais

Na LUCY MKANYIKA

SERIKALI ya Kaunti ya Taita Taveta imetishia kuwasilisha malalamishi kwa Rais Uhuru Kenyatta kuhusu usimamizi wa mbuga ya wanyama ya Tsavo, baada ya mashauriano kati ya kaunti hiyo na Wizara ya Utalii kugonga mwamba.

Miezi sita iliyopita, mahakama ilitupa nje kesi ambapo kaunti hiyo ilishtaki serikali ikitaka sehemu ya mapato yanayokusanywa katika mbuga hiyo, ikaamuliwa suluhu itafutwe kupitia mashauriano.

Waziri wa Ardhi katika kaunti hiyo, Bw Mwandawiro Mghanga, alilaumu wizara kwa kutojitolea kufanikisha mashauriano.“Tumesafiri hadi Nairobi mara mbili na maafisa wa wizara wameshindwa kuhudhuria mkutano. Hiyo inaonyesha wazi hawachukulii suala hili kwa uzito,” akasema.

Hata hivyo, naibu mkurugenzi wa mawasiliano katika wizara hiyo, Bw Maina Kigaga alisema suala hilo linashughulikiwa na Shirika la Kuhifadhi Wanyamapori (KWS).Katika mahojiano ya awali, Waziri wa Utalii, Bw Najib Balala, alishauri kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Granton Samboja, ishirikiane na serikali ya kitaifa kusimamia mbuga hiyo ya wanyama badala ya kupigania mgao wa mapato.

Alisema usimamizi wa mbuga ya wanyama kama hiyo huhitaji rasilimali tele na hilo linaweza kulemea serikali ya kaunti.

You can share this post!

Chager aashiria kushindwa

Siku Mudavadi, Kalonzo ‘walitekwa nyara’ na wanakijiji

T L