Habari Mseto

Kaunti yawapa wakulima mbegu za kahawa kwa bei nafuu

December 14th, 2018 1 min read

Na KNA

SERIKALI ya Kaunti ya Baringo imeanzisha mpango wa kuwapa wakulima mbegu za kahawa kwa bei nafuu zenye thamani ya Sh4.5 milioni kama mbinu ya kupanua kilimo cha zao hilo.

Gavana Stanley Kiptis alisema serikali yake, kupitia idara ya Mifugo na Kilimo imenunua miche ya kisasa ipatao 89,000 na mifuko 1,500 ya fatalaiza aina ya NPK kusambaziwa wakulima wa kahawa katika kaunti yake.

Akihutubu katika sherehe za Jamhuri Dei katika uwanja wa Shule ya msingi ya Moi Kabartonjo, gavana huyo alisema kando na kuwekeza zaidi kwa sekta hiyo, serikali yake pia itawapa wakulima maafisa zaidi wa kilimo ili wapata mafunzo bora ya kilimo cha zao hilo.

Alisema kaunti yake inaangazia mbinu za kuuza kahawa moja kwa moja kwa soko la Korea Kusini baada ya kujenga kituo cha kusaga.

Gavana Kiptis alipuuzilia mbali uvumi kwamba mradi wa Sh100 milioni uliopangiwa kujengwa eneo la Katimok umehamishiwa Eldama Ravine, Koibatek.

Alisema imekuwa vigumu kujenga kituo hicho katika msitu wa Katimok kama ilivyopangwa kwani sheria hairuhusu shirika la Huduma za Misitu kutenga ardhi kwa matumizi ya viwanda.

“Kwa sasa tunashauriana na Korea na washikadau wengine kuhusu  suala hili, ili kusaka eneo tofauti,” akaelezea.

Ujenzi wa kiwanda cha kahawa uliasisiwa na aliyekuwa gavana Benjamin Cheboi hapo Aprili 13, 2017 katika msitu wa Katimok.