Kaunti za eneo la Ziwani kuelimisha jamii kuhusu Ebola

Kaunti za eneo la Ziwani kuelimisha jamii kuhusu Ebola

NA ELIZABETH OJINA

KAUNTI za maeneo yanayopakana na Ziwa Victoria zimeimarisha mpango wa kuchunguza na kutoa uhamasisho kuhusu ugonjwa wa Ebola.

Hatua hiyo inajiri baada ya kuibuka kwa ripoti kwamba mgonjwa mmoja alionyesha dalili za ugonjwa huo katika kaunti ya Kakamega.

Hata hivyo, Wizara ya Afya imesema sampuli za mgonjwa huyo zilipimwa katika maabara ya Taasisi ya Utafiti wa Kimatibabu (Kemri) na kubainika kuwa hazina virusi vya Ebola.Katika kaunti ya Kisumu, uchunguzi wa virusi vya Ebola umeimarishwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kisumu.

Uhamasisho kuhusu ugonjwa huo pia umeshika kasi katika fuo zilizoko kando ya Ziwa Victoria.

Kulingana na Afisa wa Mawasiliano kaunti ya Kisumu John Oywa, Idara ya Afya imewatuma maafisa wake katika uwanja huo wa ndege kuwachunguza abiria waliotoka Uganda kupitia uwanja wa ndege wa Entebbe.

“Tumeimarisha uhamasisho na uchunguzi katika fuo za Ziwa Victoria. Wakati huu tunatayarisha wadi maalum za kuwahudumia wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH),” akasema Bw Oywa.

Mwenyekiti wa Muungano wa Kiuchumi wa Eneo la Ziwa (LREB) Profesa Khama Rogo pia alitoa wito kwa serikali za kaunti za eneo hilo kuwa chonjo kuchunguza visa vya Ebola.Mlipuko wa ugonjwa huo umeripotiwa nchini Uganda na kufikia jana jumla ya watu 20 walikuwa wameambukizwa ugonjwa huo.

“Ipo haja kwa ripoti kutolewa haraka kuhusu watu wenye dalili za ugonjwa huo ili watengwe na kutibiwa,” akasema Profesa Rogo.

“Huu ni wakati mgumu kwetu kwa sababu ni kipindi cha mpito katika serikali ya kitaifa na serikali za kaunti. Jinsi mnavyofahamu kaunti nyingi zina magavana wapya,” akaongeza.

Hata hivyo, Profesa Rogo alionya tahadhari za haraka zisipochukuliwa hali hiyo ya mpito inaweza kutoa mwanya kwa maambukizi.

Katika kaunti Trans Nzoia, Gavana George Natembeya amewaagiza wasimamizi wa mochari kutopokea maiti kutoka Uganda.

Aidha, gavana huyo amewatuma maafisa wa matitabu katika eneo la mpakani la Suam kuwakagua watu wanaoingia nchini.Kaunti kaunti ya Busia raia wanatumia njia za vichochoro kuingia Uganda na kujiweka katika hatari ya kuambukizwa Ebola.

Jana Jumapili, raia katika mji wa Busia walionekana wakiendelea na shughuli zao kama kawaida huku baadhi yao wakivuka mpaka na kuingia taifa hilo jirani na kurejea Kenya.

Wafanyabiashara kutoka Kenya na Uganda wamekuwa wakitumia njia za vichochoro kuepuka kugunduliwa na maafisa wa afya na maafisa wa usalama.

Hata hivyo, afisa wa afya Dkt Melsa Lutomia alisema kuwa maafisa wake wamekuwa chonjo tangu mkurupuko wa Ebola kugunduliwa nchini Uganda.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Waraka kwa wanaume: Ni aibu kudhulumu...

Kibarua cha Raila kulinda ufuasi Gusii

T L