Habari Mseto

Kaunti za Mlima Kenya na Pwani zaburuta mkia kwa utendakazi

October 29th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

KAUNTI za Kakamega, Kwale na Makueni zinazoongozwa na magavana Wycliffe Oparanya, Salim Mvurya na Kivutha Kibwana mtawalia, jana zilitajwa na ripoti ya utafiti ya kampuni ya Infotrak kuwa bora zaidi katika utekelezaji wa ugatuzi.

Kaunti ya Kakamega ilizoa alama ya asilimia 57.2, ikifuatwa na Kwale kwa asilimia 54.8 huku Makueni ikipata asilimia 54.7.

Akitoa ripoti hiyo jijini Nairobi jana, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo Bi Angela Ambitho, alisema waliangazia matokeo hayo kwa kuzingatia utendakazi wa magavana husika.

Kaunti iliyovuta mkia kwenye orodha hiyo ni Tana River (39.5), inayoongozwa na Gavana Dhadho Godhana.

Kwenye utafiti huo, kaunti za maeneo ya Kati na Pwani zilipata matokeo duni kwenye uendeshaji wa ugatuzi katika masuala mbalimbali ikilinganishwa na maeneo mengine nchini. Kaunti hizo pia zilibaki nyuma katika uendeshaji wa sekta muhimu kama kilimo, elimu na afya.

Katika orodha ya kaunti 15 bora kwenye utekelezaji wa ugatuzi, maeneo hayo yaliwakilishwa na kaunti za Kwale na Nyeri pekee.

Kaunti hizo ziliorodheshwa katika nambari mbili na 14 mtawalia, huku kiwango chake cha mafanikio katika utekelezaji wa ugatuzi kikiwa asilimia 54.8 na 49.3 mtawalia.

Kaunti ya Kakamega ndiyo iliyoorodheshwa bora kote nchini kwa kuzoa asilimia 57.2

Katika sekta ya kilimo, ni Kaunti ya Murang’a pekee kutoka Kati iliyoorodheshwa kuwa miongoni mwa kaunti 15 bora nchini katika uendeshaji wa sekta hiyo.

Hii ni licha ya kilimo kuwa kitegauchumi cha wakazi wengi katika eneo hilo. Kwale iliorodheshwa kuwa ya tisa huku Murang’a ikiibuka nambari 14. Kaunti ya Kakamega ndiyo iliyoorodheshwa kuwa bora.

Kati ya maeneo yote manane nchini kwenye uendeshaji wa kilimo, Kati iliorodheshwa namba sita huku Pwani ikishikilia nambari saba.

“Kaunti hizo zinapaswa kuongeza mikakati kuimarisha sekta muhimu zinazowaathiri wenyeji,” akasema Bi Ambitho.

Katika sekta ya afya, Kati iliibuka ya sita huku Pwani ikiibuka ya saba.

Hata hivyo, Pwani ilitia fora katika uendeshaji wa sekta ya elimu kwa kuibuka ya pili nyuma ya Magharibi. Eneo la Kati lilishikilia nafasi ya nne nayo Kaskazini Mashariki ikiwa ya saba.