Kaunti za Nairobi, Kajiado, Kiambu, Nakuru na Machakos zafungwa kuzuia corona

Kaunti za Nairobi, Kajiado, Kiambu, Nakuru na Machakos zafungwa kuzuia corona

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta ameamuru kusitishwa kwa safari za kuingia na kuondoka katika kaunti za Nairobi, Kiambu, Machakos, Kajiado na Nakuru kama njia ya kuzuia kuenea kwa Covid-19 kipindi hiki cha mkumbo wake wa tatu.

Kaunti hizo zimefungwa kwa muda wa siku 30 zijazo kufuatia ushahidi ambao unaonyesha kuwa idadi ya maambukizi imepanda kwa kiwango kikubwa mno.

“Kaunti hizo zimetambuliwa kwa pamoja kama kitovu cha maambukizi ya ugonjwa. Kwa hivyo, serikali imechukua hatua hii ili kulinda maisha ya wananchi kufuatia ongezeko la idadi ya wanaombukizwa wakati huu ambapo Kenya inashuhudia wimbi la tatu la maambukizi,” akasema Rais Kenyatta kwenye hotuba kwa taifa kutoka Ikulu ya Nairobi, Ijumaa.

Kiongozi wa taifa pia ameongeza muda wa kafyu katika kaunti hizo tano ambapo utakuwa ukianza saa mbili za usiku hadi saa kumi za alfajiri. Kafyu imekuwa ikitekelezwa kuanzia saa nne za usiku hadi saa kumi alfajiri.

Rais Kenyatta pia amepiga marufuku biashara za baa na uuzaji wa pombe katika mikahawa sawa na vikao vya ana kwa ana katika bunge la kitaifa, seneti na mabunge yote 47 ya kaunti.

“Tumelazimika kuchukua hatua hii kufuatia ongezeko la viwango vya maambukizi ya corona kutoa asilimia 2.6 mnamo Januari hadi asilimia 22 mwezi huu wa Machi. Hii ina maana kuwa kwa kila watu 100 wanaopimwa corona, watu 20 wanapatikana na virusi vya corona,” akasema Rais.

“Hali ni mbaya zaidi katika kaunti ya Nairobi ambapo inachangia asilimia 60 ya idadi jumla ya maambukizi ya corona nchini kufikia sasa. Hii ina maana kuwa kati ya watu 10 wanaopatikana na Covid-19 nchini, sita wanatoka Nairobi,” akaongeza Rais Kenyatta.

Kiongozi wa taifa pia amepiga marufuku mikutano yoyote ya kisiasa katika kaunti za Nairobi, Kiambu, Kajiado, Nakuru na Machakos hadi wakati usiojulikana.

Rais Kenyatta pia amepiga marufuku ibada za ana kwa ana ndani ya kaunti hizo tano ambazo zimefungwa.

Katika kaunti 42 kafyu itaendelea kutekelezwa kwa muda wa kawaida wa kuanzia saa nne za usiku hadi saa kumi za alfajiri huku wakazi wa kaunti hizo wakitakiwa kuendelea kuzingatia masharti ya kawaida ya kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Kuhusu hafla za mazishi na harusi, Rais Kenyatta ameamuru kuwa yahudhuriwe na watu wasiozidi 100 lakini ambao watazingatia masharti dhidi ya corona. Mikutano ya kijamii nayo imewekwa kuhudhuriwa na watu 15 pekee.

Rais Kenyatta pia amepiga marufuku shughuli zote za michezo na masomo ya ana kwa ana isipokuwa wanafunzi wanaofanya mitihani ya kitaifa.

You can share this post!

Serikali yafafanua kuhusu ‘lockdown’ ya...

Watu 2,008 wapatikana na corona Kenya kipindi cha muda wa...