Habari MsetoSiasa

Kaunti zinadaiwa Sh100 bilioni na wanakandarasi – KNCCI

August 4th, 2019 2 min read

GEORGE MUNENE na CAROLINE WAFULA

SERIKALI za Kaunti zinadaiwa jumla ya Sh100 bilioni na wanakandarasi, haya ni kwa mujibu wa wa kiongozi wa Chama cha Wafanyabiashara nchini (KNCCI) Richard Ngatia.

Bw Ngatia jana alishutumu magavana kwa kuchelewa kuwalipa wanakandarasi waliopata zabuni za kuendeleza miradi mbambali na kusambaza huduma na bidhaa kwa serikali za kaunti.

Akizungumza jana katika shule ya Msingi ya Kanjuu, Kaunti ya Kirinyaga katika tamasha ya kitamaduni, Bw Ngatia alisema kuwa wanakandarasi wanahangaika kutokana na kucheleweshwa kwa malipo yao.

Alisema baadhi ya wanakandarasi wameshindwa kulipa mikopo ya benki kwa sababu serikali za kaunti ‘zimekwama’ na hela zao.

“Wanakandarasi walikopa fedha kutoka kwa taasisi za kifedha. Kucheleweshwa kwa malipo yao kunamaanisha kwamba wanapigwa faini na hawataweza kupata mikopo katika siku za usoni,” akaongezea.

Wakati huo huo, Baraza la Magavana (CoG) limemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati na kutatua utata kuhusu ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti.

Mwenyekiti wa CoG Wycliffe Oparanya alimlilia Rais Kenyatta akisema kuwa ana uwezo wa kutatua mkwamo huo ili kuwezesha serikali za kaunti kupokea fedha mapema.

Bw Oparanya alisema mvutano uliopo baina ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu mgao wa fedha kwa serikali za kaunti umetatiza shughuli za maendeleo katika kaunti.

Alifananisha mzozo huo na mapigano baina ya fahali wawili ambapo nyasi ndizo huumia.

“Rais Kenyatta anafaa kuwa refarii wa kupatanisha maseneta na wabunge,” akasema Bw Oparanya Jumamosi wakati wa mazishi ya aliyekuwa gavana wa Bomet Dkt Joyce Laboso katika eneo la Koru, Kisumu.

“Kwa sasa tuna fahali wawili wanaopigana; Bunge la Kitaifa na Seneti. Sisi magavana ndio tunaumia. Wewe ndiye refarii na una uwezo wa kuingilia kati na kumaliza mvutano uliopo,” akaongeza Gavana huyo wa Kakamega.

Alimtaka Rais Kenyatta kuagiza Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen na mwenzake wa Bunge la Kitaifa Adan Duale kuhakikisha kuwa wanatatua mvutano uliopo ili kuwezesha serikali za kaunti kupokea fedha zao.

“Serikali za kaunti zinakusihi, kukutana na Bw Murkomen na Bw Duale ili suala hili kuhusu mgao wa fedha kwa kaunti litatuliwe,” akasema.

Bunge la Kitaifa linataka serikali za kaunti zipewe Sh316 bilioni. Lakini maseneta wameshikilia kuwa serikali za kaunti zipewe mgao wa Sh335 bilioni.

Rais Kenyatta wiki mbili zilizopita alizitaka serikali za kaunti kukubali Sh316 bilioni akisema kuwa serikali ya kitaifa haina fedha zaidi.

“Ikiwa maseneta wanataka kuzipa kaunti Sh335 bilioni wakate mishahara yao wawape. Mimi sina fedha,” akasema Rais Kenyatta alipokuwa akihutubia waombolezaji wakati wa mazishi ya mama ya aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth.

Magavana tayari wamewasilisha kesi katika Mahakama ya Juu wakitaka mahakama iwaruhusu kupewa sehemu ya fedha kuepuka kukwama kwa shughuli za kaunti.

Jaji Mkuu David Maraga ameshauri pande zinazozozana kujadiliana na kuelewana nje ya mahakama.