Habari Mseto

Kaunti zafutilia mbali ada za mochari kupiga jeki vita dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona

March 25th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI kadha za kaunti nchini sasa zimeondoa ada ambazo mochari hutoza ili kuziwezesha familia zilizofiwa kuzika miili haraka.

Hatua kama hii itapunguza uwezekano wa kuwepo kwa mikutano mingi ya kupanga mazishi na hivyo kuvutia watu wengi.

Kaunti za Kakamega na Uasin Gishu ndizo zilikuwa za kwanza kufutilia mbali ada hizo wiki jana kama sehemu ya hatua ya kupunguza kuenea kwa virusi vya corona.

Na Jumanne, serikali ya Kaunti ya Nairobi iliiga mfano huo kwa kutoa ilani ya siku saba kwa familia mbalimbali kuchukua miili ya wapendwa wao, bila malipo, kutoka hifadhi ya maiti ya City ili zikaizike.

Ada hizo pia zimefutuliwa mbali mbali hifadhi ya maiti zilizoko katika hospitali zingine zilizoko chini ya usimamizi wa serikali ya kaunti ya Nairobi.

Waziri wa Afya katika Kaunti ya Naironi Hitan Majevda alisema ni miili ambayo ingali inafanyiwa uchunguzi na polisi itasalia katika hifadhi hizo za maiti.

“Watu ambao miili ya jamaa zao iko katika hifadhi za maiti wanashauri kuitambua na kuichukua kabla ya Machi 31, 2020. Wasipofanya hivyo, serikali ya kaunti itasaka kibali cha kuizika katika makaburi ya pamoja,” akasema kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Majevda alisema hatua hiyo imechukuliwa kwa lengo la kupunguza msongamano katika hifadhi za maiti jijini.

Na mnamo Jumatatu serikali ya Kaunti ya Makueni ilitoa ilani kuwa miili yote iliyoko katika hifadhi za maiti za kaunti hiyo ichukuliwe ndani ya saa 48.

“Miili hii isipochukuliwa tutawasilisha ombi la kuizika kulingana na Sheria ya Afya ya Umma,” ikasema taarifa kutoka serikali hiyo.

Huku kaunti hiyo ikiondoa ada za hifadhi za maiti iliagiza familia husika kwamba mazishi yanafaa kuhudhuriwa na watu wa familia pekee; na wasiozidi idadi baina ya 10 na 15.