Habari

Kaunti zajitahidi kulipa wafanyakazi mishahara

August 14th, 2019 1 min read

Na WAANDISHI WETU

SERIKALI za kaunti katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa Jumanne zilizuia kufanyika kwa mgomo wa wafanyikazi kwa kuahidi kuwalipa wiki hii.

Ahadi hiyo ilifuatia majadiliano kati ya maafisa wa kaunti husika na wale wa muungano wa wafanyakazi.

Katibu wa muungano huo wa wafanyakazi Joseph Cheruiyot alifichua kuwa usimamizi wa kaunti umeanza shughuli ya kuwalipa wafanyakazi kufikia kesho.

Kwenye makubaliano hayo, kaunti zitalipa mishahara ya Julai katika muda wa siku mbili zijazo.

Kaunti hizo ni Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet na Baringo.

Nazo zile za Nandi, Trans Nzoia na Turkana ziliwalipa wafanyakazi wao wiki iliyopita.

Mishahara hiyo imechelewa kutokana na mvutano kati ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu Mswada wa Ugavi wa Mapato 2019.

Gavana wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Alex Tolgos alikutana na waakilishi wa muungano wa wafanyakazi na kufanya mkataba kuhusu malipo ya mishahara iliyocheleweshwa.

Aliahidi kufanya malipo hayo kabla ya mwisho wa wiki hii.

Katibu wa Tawi la Muungano wa Kitaifa wa Wauguzi, Patrick Biwott, aliwahimiza magavana kulipa mishahara ili kuwakinga wafanyakazi dhidi ya changamoto zaidi za kifedha.

Serikali ya Kaunti Baringo pia iliahidi kufanya malipo hayo wiki hii.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulifichua kwamba shughuli zilikuwa zikiendelea vyema katika hospitali ya rufaa ya Kaunti ya Baringo na idara nyinginezo.

Katika eneo la Uasin Gishu, kaunti ilifanya mkataba na wafanyikazi ikiahidi kuwalipa.