Habari

Kaunti zakwama

July 6th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

HUDUMA katika kaunti zote 47 nchini huenda zikakwama iwapo Wizara ya Fedha itaendelea kuchelewesha pesa ilizopaswa kuwapa magavana mwezi Juni.

Baraza la Magavana linasema kwamba serikali za kaunti hazina pesa baada ya Wizara ya Fedha kuchelewa kutoa Sh43 bilioni za kuendesha huduma ilizopaswa kutoa mwaka 2018.

Hayo yanajiri huku mzozo kati ya Seneti na Bunge kuhusu mgao wa pesa ambazo serikali hizo zinapaswa kutengewa kwenye bajeti ya mwaka huu ukiendelea.

Kufikia Ijumaa, wafanyakazi vibarua wanaotoa huduma muhimu katika serikali za mashinani hawakuwa wamepata mishahara ya Juni.

Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Bw Wycliffe Oparanya alisema serikali za kaunti zinahangaika kuendesha shughuli zake.

Bajeti ya mwaka huu ilisomwa kabla ya mabunge hayo mawili kuafikiana mgao ambao serikali za kaunti zinapaswa kutengewa; hatua ambayo inaongeza masaibu katika serikali hizo zinazozongwa na madeni.

Kulingana na Bw Oparanya, hatua ya wizara ya fedha kukosa kupatia serikali za kaunti pesa kwa wakati na mzozo kati ya seneti na wabunge zitalemaza huduma katika serikali hizo.

“Mzozo kuhusu suala hili unaathiri vibaya huduma katika serikali za kaunti na unapaswa kutatuliwa haraka,” alisema Bw Oparanya.

Alisema kwamba serikali za kaunti zilitarajia pesa mwishoni mwa wiki hii na zikikosa kutolewa huduma zitatizika.

“Nimefahamishwa kwamba mazungumzo yanaendelea na kwamba Bunge la Taifa linapendekeza kaunti zitengewe Sh319 bilioni ilhali baraza la magavana lilipendekezea seneti Sh327 bilioni,” alisema Bw Oparanya.

Mzozo kuhusu suala hilo umefufua uhasama kati ya seneti na Bunge la Taifa, wabunge wakitaka seneti ivunjwe nao maseneta wakiapa kushtaki bunge.

Ugatuzi hatarini

Wadadisi wanasema mzozo huu unaweza kusambaratisha ugatuzi ambao umefaidi pakubwa sehemu zote nchini.

Japo kaunti nyingi nchini wiki hii ziliwasilisha bajeti katika mabunge ya kaunti zao na ikaidhinishwa, huenda miradi yote iliyonuiwa ikayumba iwapo Bunge la Taifa na Seneti hazitatatua mvutano uliopo.

Kulingana na Bw Oparanya, mwezi wa Juni ambao ni wa mwisho wa mwaka uliopita wa matumizi ya pesa za serikali, Kaunti hazikupata pesa.

“Ni muhimu Wakenya wafahamu kwamba, serikali za kaunti hazina pesa za kutekeleza majukumu yake na huduma zitakwama,” alisema Bw Oparanya mnamo Juni 19 alipohutubia wanahabari jijini Nairobi.

Kulingana na Bw Oparanya, sekta ambazo zitaathiriwa ni afya huku kaunti zikidaiwa mabilioni na Shirika la kusambaza dawa nchini (KEMSA).

Shirika hilo limeonya kuwa halitaweza kupatia serikali za kaunti dawa kabla ya kulipa deni la jumula ya Sh5 bilioni.

Sekta ambazo serikali za kaunti zinasema zitakwama iwapo hazitapata pesa kutoka kwa serikali kuu ni kilimo ambayo magavana wanalenga kutumia Sh5 billioni kuwapa wakulima mbolea ya bei nafuu, huduma za kuwapa wakazi maji safi ya kunywa iliyotengewa jumula ya Sh10 bilioni, miundomisingi (Sh35 bilioni) na shughuli za kuendesha serikali za kaunti (Sh45 bilioni).