BRIAN OCHARO NA STEPHEN ODUOR
MAGAVANA wa ukanda wa Pwani wameitaka serikali ya kitaifa kuelekeza mabilioni ya fedha inayotengewa miradi ya uchumi wa baharini, kwa serikali za kaunti za eneo hilo watekeleze miradi inayolengwa.
Kulingana nao, pesa nyingi huwekwa katika miradi ya uchumi wa baharini na serikali kuu, ilhali hakuna matunda yanayoonekana mashinani.
Uchumi wa baharini ambao unahusu utumizi bora wa rasimali za majini, ni sekta ambayo imekuwa ikipewa uzito kimataifa kwa miaka kadhaa sasa.
Hii imefanya mashirika ya kimataifa pamoja na serikali kutenga mabilioni ya pesa kila mwaka kwa lengo la kukuza sekta hiyo.
Wakizungumza Jumatano wakati wa kongamano la nne la uwekezaji wa kiuchumi katika kilimobiashara la Jumuiya ya Kaunti za Pwani mjini Hola, Kaunti ya Tana River, magavana wa Pwani walisema mahitaji ya sekta hiyo yamo chini ya serikali za kaunti Kikatiba.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na magavana Dhadho Godhana wa Tana River, Andrew Mwadime (Taita Taveta), Issa Timamy (Lamu) na Gideon Mung’aro (Kilifi).
Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani na mwenzake wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, hawakuhudhuria.
“Uchumi wa baharini umegatuliwa. Kwa hivyo serikali ya kitaifa haipaswi kujihusisha na utekelezaji wake. Serikali inapaswa izipe kaunti husika fedha ili zitekeleze miradi yao,” akasema Bw Timamy.
Kulingana naye, wananchi wangekuwa sasa wanafurahia maendeleo mengi iwapo sekta hiyo ingekabidhiwa kikamilifu kwa serikali za kaunti.
“Tunataka kuona maendeleo nyanjani. Miradi ambyo itabadilisha maisha ya watu wa Pwani,” aliongeza gavana Timamy.
Hata hivyo, Bw Mung’aro ambaye ndiye Mwenyekiti wa JKP alieleza matumaini kwamba uwepo wa wizara ya uchumi wa baharini huenda ukaleta mabadiliko.
Wizara hiyo inasimamiwa na gavana mstaafu wa Kwale, Bw Salim Mvurya.
“Ustawi wa sekta hii utawezekana kupitia kwa ushirikiano wa wadau wakiwemo wawekezaji wa kibinafsi. Kama magavana, tuna jukumu la kuweka mandhari bora ya uwekezaji katika kaunti zetu,” akasema Bw Mung’aro.
Gavana Mwadime alihoji kuwa kuna umuhimu wa kaunti za Pwani kuungana na kuzungumza kwa sauti moja, ili kuendeleza ajenda ya kiuchumi katika eneo hilo.
“Tufanye kazi kama timu moja ili tuongeze ushawishi wetu tunapotetea maslahi ya kaunti zetu,” alisema Bw Mwadime.
Kwa upande wake, Bw Godhana alitaka serikali ya kitaifa kuwekeza zaidi katika miradi mikubwa ya kuwasaidia wakazi wa kaunti zilizotengwa.
“Serikali inapaswa kulaumiwa kwa kuwacheleweshea watu wake maendeleo. Tumeomba vitu viwili kwa muda. Uwanja wa ndege na barabara ya kutuunganisha na jiji kuu,” alisema Bw Godhana.
Kulingana naye ni wakati wa serikali kubadili mtazamo wake kwa kaunti ya Tana River, na kuiweka katika ajenda ya maendeleo.
Viongozi hao walitoa ombi la umoja wa kaunti sita za Pwani, wakihoji kuwa kutawapa nguvu ya ushawishi, kuhusiana na masuala muhimu ya eneo hilo.
Subscribe our newsletter to stay updated