Habari Mseto

Kaunti zilifuja fedha za maendeleo kwa anasa, ziara – Ripoti

October 24th, 2020 2 min read

Na ONYANGO K’ONYANGO

RIPOTI ya Mdhibiti wa Bajeti imeonyesha kwamba serikali nyingi za Kaunti katika eneo la North Rift zimekuwa zikitumia mamilioni ya fedha kwa safari za ndani na nje ya nchi, pamoja na mishahara, badala ya kufanya miradi ya kimaendeleo, huku zikiendelea pia kupata mapato ya chini.

Ripoti hiyo inaonyesha kwamba, licha ya baadhi ya kaunti kuboresha mapato yao, zote katika eneo hilo waliamua kutumia pesa zaidi ya uwezo wao, huku baadhi ya miradi muhimu ikikwama.

Ripoti hiyo ilithibitisha kuwa kaunti hizo pia zina madeni mengi yanayoathiri shughuli zao.

Katika Kaunti ya Baringo, mnamo mwaka wa fedha wa 2019 hadi 2020, serikali hiyo ilitumia Sh1.73 bilioni badala ya Sh3.50 bilioni.

Utawala wa Gavana Stanley Kiptis ulikumbwa na mrundiko wa madeni kwa jumla Sh78.66 milioni.

“Matumizi hayo yaliwakilisha asilimia 49.4 pekee ya malengo yao ya maendeleo ya kila mwaka,” akasema Mdhibiti wa Bajeti Dkt Margaret Nyakang’o.

“Kaunti hiyo pia ilitumia Sh51.39 milioni kwa vikao vya kamati za Wawakilishi wa Wadi 45 na spika, dhidi ya mgawo wa fedha katika bajeti ya kila mwaka ya Sh79.22 milioni. Kiwango cha fedha alichokipata mwakilishi mmoja wa wadi kwa kila kikao kilikuwa Sh93,093, dhidi ya kiwango kilichopendekezwa na Tume ya Mishahara na Malipo ya jumla ya Sh124,800, kila mwezi,” akasema Dkt Nyakang’o.

Hali kama hiyo ilishuhudiwwa katika kaunti ya Elgeyo Marakwet ambapo badala ya kutumia Sh2.41 bilioni katika maendeleo, jumla ya Sh1.11 bilioni pekee zilitumika.

Kaunti hiyo pia ilitumia Sh32.31 milioni kwa vikao vya Kamati za wawakilishi wa wadi 40 na spika dhidi ya mgawo wa bajeti ya kila mwaka ya Sh49.92 milioni.

Serikali ya Kaunti ya Nandi, ilirekodi mapato ya chini ya Sh267.08 milioni, dhidi ya makadirio ya kila mwaka ya Sh628.82 milioni.

Pia, kaunti hiyo iko na madeni ya jumla ya Sh261.06 milioni kufikia Juni 30, 2020.

Kaunti ya Trans-Nzoia ni mojawapo ya kaunti ambazo zina madeni ya juu zaidi kwa jumla ikiwa Sh1.16 bilioni kufikia Juni 30, 2020.

“Pia, walipata mapato ya chini ya Sh356.08 milioni dhidi ya makadirio yao ya kila mwaka ya Sh500 milioni. Mapato yaliyopatikana yalionyesha asilimia 71.2 ya malengo yake ya kila mwaka,” alisema Dkt Nyakang’o.

Kaunti ya Uasin Gishu nayo ilikiwa na tofauti kati ya ripoti ya utekelezaji wa bajeti na programu ndogo ambazo zinaonyesha matumizi ya jumla Sh8.12 bilioni ikilinganishwa na Sh8.10 bilioni zilizonukuliwa katika ripoti ya mwaka ya kaunti.