CHARLES WASONGA: Kaunti zisipodhibitiwa nchi itaisha kwa ufisadi

CHARLES WASONGA: Kaunti zisipodhibitiwa nchi itaisha kwa ufisadi

Na CHARLES WASONGA

INAVUNJA moyo kwamba wajumbe katika Kongamano la Saba la Ugatuzi, Makueni, walipokuwa wakidurusu peo za maendeleo ambazo serikali za kaunti zimefikia tangu 2013, Kaunti ya Siaya ilikuwa inagonga vichwa vya habari kutokana na sakata ya ufisadi.

Maafisa 64 kutoka Idara ya Fedha katika kaunti hiyo wamekuwa wakidadisiwa na maafisa wa DCI kuhusiana na wizi wa karibu Sh600 milioni za umma katika serikali hiyo.

Inadaiwa kuwa wizi huo ulitekelezwa mnamo Juni mwaka huu ambapo mamilioni ya fedha yalitolewa kutoka hazina ya kaunti na kuelekezwa katika akaunti za benki za watumishi hao kuanzia wale wa ngazi za juu hadi ngazi za chini.

Inasemekana wizi huo ulikwamisha huduma muhimu katika kaunti hiyo, kama vile, ulipaji wa mishahara ya wafanyakazi na wakandarasi waliotekeleza miradi mbalimbali katika serikali hiyo.

Isitoshe, serikali ya Kaunti ya Siaya ililazimika kujiondoa kutoka mashindano ya michezo kati ya serikali za kaunti (KICOSCA) yaliyofanyika katika Kaunti ya Embu mnamo Oktoba kwa sababu ilikosa Sh16 milioni za kugharimia mahitaji ya wawakilishi wake katika michezo hiyo.

Ikumbukwe kwamba kulingana na ripoti iliyowasilishwa na Shirika la Kutwaa Mali ya Umma Iliyoibwa (ARA) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Desemba 21, 2020, asasi hizo zilikuwa zikifuatilia kesi za wizi wa zaidi ya Sh100 bilioni kutoka kwa hazina za kaunti mbalimbali nchini.

Miongoni mwa magavana wa sasa na wa zamani wanaokabiliwa na kesi za wizi wa mamilioni ya pesa za umma katika kaunti zao ni Okoth Obado (Migori, Sh300 milioni), Ali Korane (Garissa, Sh233 milioni ), Muthomi Njuki (Tharaka Nithi, Sh34 milioni), Evans Kidero (Nairobi, Sh244 milioni) na Ferdind Waititu (Kiambu, Sh236 bilioni).

Hizi ni pesa ambazo zingetumika kufadhili ujenzi wa barabara, shule za chekechea, vituo vya afya, masoko, viwanja vya michezo, kati ya miradi mingine ya maendeleo.

Isitoshe, pesa hizo zingetumiwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo maeneo ya mashambani ambavyo vina uwezo wa kuzisaidia serikali za kaunti kujiongezea mapato na kutoa nafasi za ajira kwa wakazi.

Nimetoa mifano hii ili kuhimili tasnifu yangu kwamba japo kaunti nyingi zimepiga hatua kimaendeleo tangu mfumo wa ugatuzi ulipoanza kutekelezwa nchini miaka minane iliyopita, ufisadi ni doa katika ufanisi huu.

Kwa hivyo, ingawa kauli mbiu katika Kongamano la Ugatuzi la mwaka huu ilikuwa ni mikakati ya kupambana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, hayo hayawezi kufikiwa endapo ufisadi utazidi kuchukuliwa kama jambo la kawaida katika kaunti zetu.

Serikali za kaunti hazitafaidi kutokana na ufadhili wa Sh7 bilioni ambazo Rais Uhuru Kenyatta aliziahidi kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwa magavana hawatajitolea kuongoza vita dhidi ya ufisadi katika serikali zao.

Naamini kuwa miaka minane baada ya mfumo wa ugatuzi kuanza kutekelezwa nchini, serikali zote 47 zinaweza kukusanya mapato ya kutosheleza mahitaji yao bila kutegemea mgao wa fedha kutoka Serikali ya Kitaifa.

Kwa mfano, kaunti za maeneo ya kaskazini mwa Kenya kama vile Isiolo, Turkana, Baringo, Pokot Magharibi, Marsabiti, Samburu na Wajir zinaweza kustawisha sekta ya ufugaji ili kujitosheleza kimapato. Hii ni ikiwa magavana na maafisa wao watakumbatia maadili katika utendakazi wao.

  • Tags

You can share this post!

Dhuluma za ngono zinavyotatiza utalii

Jinsi maafisa, viongozi walihusika katika sakata ya uuzaji...

T L