Makala

Kawi ya jua inavyoboresha maisha ya wakazi wa mashambani

August 22nd, 2019 3 min read

 NA RICHARD MAOSI

Jeniffer Achieng anatumia kiti chake kufikia paneli za kawi ya jua, zilizowekwa kwenye paa la nyumba yake.

Akiwa amezishikilia kwa uangalifu, anaelezea jinsi maisha yake yalivyobadilika katika kijiji cha Kabonyo, Kaunti ya Kisumu, kilomita kadhaa kutoka kwenye transfoma ya kusambaza umeme.

“Awali nililazimika kutumia hela nyingi kununua mafuta taa, wakati mwingine kama sina pesa ilinibidi kutumia kuni ili kutimiza shughuli za nyumbani,” anasema Bi Acieng, 65, nyanya wa wajukuu watano.

Wajukuu wake wanafurahia masomo yao kwani wao hufanya kazi ya ziada kwa wakati kabla ya kwenda kulala  kwa ajili ya mapumziko, bila hofu ya umeme kupotea.

Mara nyingi alikuwa akimtuma mjukuu wake kumpelekea simu yake ili ipate chaji, kilomita sita kutoka nyumbani, jambo lililompa taabu hasa umeme unapokatika na kumfanya asubiri hadi siku inayofuata.

Kwa upande mwingine, Mercy Kalondu, mkazi wa Kasikeu, Kaunti ya Makueni anaelezea jinsi teknolojia mpya ya televisheni ilivyomfaa kupata burudani nyumbani.

“Ingawa nimeunganishiwa umeme, visa vya stima kupotea mara kwa mara, vilinifanya kuvumilia matatizo ya kutotazama runinga, kusikiliza redio na kuchaji simu. Lakini tangu ninunue televisheni inayowezeshwa na sola ninaweza kupata burudani mbali na kuwasha taa katika jumba langu lenye vyumba vitano,” anasimulia mama huyo wa watoto watatu.

Kulingana na wachanganuzi wa maswala ya kawi, miundomsingi duni barani Afrika imekuwa kizingiti kikubwa kwa usambazaji wa umeme, na kuzima maendeleo ya kiuchumi.

Ndio sababu serikali ya kitaifa imeanzisha juhudi za kusambaza umeme mashinani, ili kuongeza idadi ya watu wanaotumia stima ifikapo 2020.

Wakenya kama vile Bi Achieng na Bi Kalondu, wanatumika kama kielelezo kwa wanawake wanaotumia njia mbadala kupata umeme, kupitia mfumo wa sola wa bei nafuu.

“Ninalipia sola yangu Sh100 kila Ijumaa, na kabla ya hapo nilitozwa Sh1,000 na kampuni ya Greenlight Planet,” Bi Achieng anasema.

Kwa upande mwingine Bi Kalondu anasema ingawa wazo la kufikisha umeme mashinani ni zuri, kuna baadhi ya maeneo ambayo hayawezi kufikika. Pia wakazi wamezoea kusafiri mwendo mrefu mashambani wakitafuta sehemu ya kuweka chaji katika rununu zao.

“Kupotea kwa stima mashinani ni jambo la kuudhi mno, kwa mfano, unaweza kuwa ukitazama habari au kipindi unachokipenda kwenye runinga halafu umeme unatoweka. Pia mara nyingi ni vigumu kuwasiliana na wapendwa wakati ambao umeme umepotea,” alisema.

Alinunua televisheni aina ya Sun King Hom 400, kutoka kwenye kampuni ya Greenlight yapata miezi mitano iliyopita. Hii inajumuisha paneli za sola, runinga ya inchi 19, 24 au 32 pamoja na king’amuzi (decoder) redio, kitambuzi na taa zinazoweza kuleta mwangaza kwenye vyumba vitano.

“Tuliskia kilio cha wanunuzi wetu ndipo tukabuni njia kabambe za kuwapa kawi safi, taa zetu zinaweza kufanya kazi kwa miaka mitano mtawalia bila matatizo yoyote,” anasema mkurugenzi wa mauzo ya Green light Planet Bw Patrick Muriuki kwenye mahojiano na Taifa Leo Dijitali.

Alisema uvumbuzi huo utawafanya watu mashinani kununua bidhaa zao kwa njia isiyokuwa na masharti mengi, ambapo sehemu ya malipo hutolewa mwanzoni huku zile zilizosalia zikilipwa baina ya miezi 1-18.

“Malipo yanaweza kufanyika kila siku, wiki au mwezi kulingana na thamani ya bidhaa, kuna zile zinazotolewa thamani ya Sh400 kwa taa na Sh1500 kwa televisheni za sola,”anasema Bw Muriuki akitaja kampuni inamiliki matawi 74 kote nchini.

Ili kuwawezesha akina mama, kampuni ya Greenlight ina wauzaji 5800 kote nchini, ambapo 2000 ni wanawake ambao wameonyesha ukakamavu kutengeneza jina la kampuni ambayo kufikia sasa.

“Wanawake ni nguzo muhimu katika familia zetu, kuna baadhi yao ambao wamechukua majukumu ya kuhudumu kama akina baba na kubadilisha jamii,” Bw Muriuki alisema akiwapongeza kwa kuchagua mfumo wa sola kwa ajili ya matumizi ya kila siku.

Aidha anasema kampuni yao imefanikiwa kuzingatia sheria ya kutoa nafasi za kazi, kwa kuajiri asilimia 50 ya wafanyikazi ambao ni wa jinsia ya kike katika kampuni yao.

“Mbali na kuishi maisha magumu ya kijijini ninaelewa changamoto wanazopitia watu wa mashambani. Tunafanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha tunawafikia watu bilioni 1.2 kote duniani, lakini hususan wale wanaoishi mashambani huku wakitumia mafuta taa ambayo ni hatari kwa usalama wao,” akasema.

Utafiti unaonyesha kuwa akina mama wnaotumia mafuta taa wako hatarini zaidi ya mara tisa kupata maambukizi ya maradhi ya pumu.

Aidha taa zinazotumia mafuta ya taa hupata ajali mbaya inayoweza kuteketeza makazi ya watu na hata kusababisha vifo kwenye mitaa ya mabanda.

Pia watoto wengi hawapati muda wa kutosha kutekeleza masomo yao, wengi wao wakiwa ni wasichana wanaoagana na masomo kutokana na kuongezeka kwa majukumu wanayofanya nyumbani.

“Vifaa vya Sun King Lights vinaweza kuongeza asilimia 75 ya muda wa kawaida wa kusoma, ambao ni saa tatu zaidi ya ya wanafunzi wanaoendeleza masomo yao nyakati za usiku,”

Nyumba zaidi ya milioni 9.5 kote ulimwenguni zimejitenga na mfumo wa kutegemea stima ya kawaida, na kubadilisha maisha ya watu milioni 48.9. Sola hutoa kiwango kidogo cha gesi ya Carbon (IV) Oxide na hivyo basi kuhakikisha kuna kiwango kizuri cha hewa safi kila wakati.