Michezo

KAZI BADO: Kutoka sare kwachelewesha sherehe Liverpool

November 29th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

SHEREHE za Liverpool na Chelsea katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya zilicheleweshwa hadi mwezi ujao baada ya kutoka sare dhidi ya Napoli na Valencia mtawalia katika mechi za makundi mnamo Jumatano.

Mabingwa watetezi Liverpool walipoteza nafasi ya kufuzu kabla ya mechi yao ya mwisho dhidi ya Salzburg itakayochezwa Desemba baada ya kukabwa 1-1 na Napoli uwanjani Anfield nao Chelsea wakatoka 2-2 dhidi ya Valencia nchini Uhipania.

Liverpool na Chelsea sasa zitaingia mechi zao za mwisho mwezi Desemba zikiwa na presha. Liverpool, ambayo inaongoza Kundi E kwa alama 10, ilijipata chini bao moja wakati wa mapumziko baada ya Dries Mertens kumwaga kipa Allison dakika ya 21.

Vijana wa kocha Jurgen Klopp walisawazisha 1-1 kupitia kwa Dejan Lovren dakika ya 65 kutokana na kona iliyochotwa vyema na James Milner na kukamilishwa kwa ustadi kupitia kichwa cha beki huyo wa Croatia.

Napoli ya kocha Carlo Ancelotti iko alama moja nyuma ya Liverpool nayo Salzburg imevuna alama saba katika nafasi ya tatu. Timu zitakazomaliza katika nafasi mbili za kwanza zitatinga raundi ya 16-bora kumaanisha kuwa kazi ya kuwania tiketi hizo mbili bado ipo.

Genk, ambayo iko mkiani kwa alama moja, tayari imeondolewa mashindanoni. Timu itakayokamilisha mechi za makundi za Klabu Bingwa katika nafasi ya tatu, itaingia mashindano ya daraja ya pili, ambayo ni Ligi ya Uropa.

Mabingwa watetezi wa Ligi ya Uropa, Chelsea walipigana kufa-kupona hadi wakaokota alama moja dhidi ya Valencia, ingawa watahitaji kuchapa Lille katika mechi ya mwisho ya Kundi H ili kujihakikishia nafasi ya kusalia katika Klabu Bingwa.

Carlos Soler aliweka wenyeji Valencia kifua mbele dakika ya 40. Hata hivyo, kabla ya Valencia kumaliza kusherehekea bao hilo, Mateo Kovacic alisawazisha dakika ya 41.

Christian Pulisic kisha alipatia Chelsea uongozi 2-1 dakika ya 50 kabla ya Daniel Wass kuweka hai matumaini ya Valencia kusonga mbele alipofuma wavuni bao la pili zikisalia dakika nane mechi itamatike.

Ajax yaongoza

Ajax kutoka nchini Uholanzi inaongoza kundi hili kwa alama 10.

Mabingwa hawa mara nne wa Klabu Bingwa Ulaya wanahitaji alama moja dhidi ya Valencia katika mechi yao ya mwisho kusalia katika mashindano hayo ya daraja ya juu.

Valencia na Chelsea wako sako kwa bako kwa alama nane kila mmoja, ingawa Valencia wako juu yao kwa sababu ya takwimu za ana kwa ana.

Hata hivyo, Chelsea inaonekana itakuwa na mtihani rahisi katika mechi yake ya mwisho dhidi ya Wafaransa Lille uwanjani Stamford Bridge. Lille bado hawajaonja ushindi msimu huu katika dimba hili.

Kufikia sasa, timu ambazo zimefuzu kushiriki mechi za raundi ya 16-bora ni Paris Saint-Germain, Real Madrid (Kundi A), Bayern Munich, Tottenham (Kundi B), Manchester City (Kundi C), Juventus (Kundi D), Barcelona (Kundi F) na Leipzig (Kundi G).