Michezo

KAZI BADO: Ole Gunnar asema mapenzi yake ni kuona Manchester United ikitoa ushindani mkali EPL

August 13th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

MANCHESTER City, Liverpool na Manchester United ndio waliotia fora zaidi katika wiki ya kwanza ya kivumbi cha Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) huku wakufunzi Steve Bruce na Frank Lampard wakipoteza michuano ya kwanza wakisimamia vikosi vyao vipya.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walianika ukubwa wa kiu ya kutetea ufalme wa taji la EPL msimu huu kwa kuwatandika West Ham United 5-0 mnamo Jumamosi huku Man-United wakiwaponda Chelsea 4-0 uwanjani Old Trafford mnamo Jumamosi.

Awali, Liverpool ya kocha Jurgen Klopp waliwanyeshea limbukeni Norwich City 4-1 mnamo Ijumaa huku Tottenham Hotspur wakiwapepeta Aston Villa 3-1 mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.

Ni matokeo ambayo yanaashiria ukali wa vita vya ushindani kati ya vikosi vilivyotawala nafasi sita za kwanza kileleni mwa jedwali msimu jana.

Wakinolewa na kocha Bruce, chombo cha Newcastle United kilizamishwa na Arsenal ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya saba.

Licha ya kusajili ushindi mnono dhidi ya Chelsea ambao kwa sasa wananing’iniza padogo mustakabali wa Lampard uwanjani Stamford Bridge, kocha Ole Gunnar Solskjaer wa Man-United amesema kwamba kikosi chake kingali na kazi kubwa ya kufanya.

Baada ya Chelsea kubusu mwamba wa goli la Man-United mara mbili, Man-United walibahatika kupata bao la uongozi kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza kupitia penalti ya mvamizi Marcus Rashford.

“Bado hatujafikia hata katikati ya safari yetu ya kujisuka upya. Tunajishughulisha vilivyo ili kupata mfumo utakaowarejesha Man-United kileleni mwa jedwali. Ingawa bado tunahitaji muda, naamini kwamba wakati huo utawadia hivi karibuni,” akasema Solskjaer.

Chini ya Solskjaer, Man-United walikamilisha kampeni za EPL msimu jana katika nafasi ya sita huku pengo la alama 32 likitamalaki kati yao na Man-City waliohifadhi ubingwa.

Fahari

Japo kubwa zaidi katika maazimio ya Man-United msimu huu ni kukamilisha kampeni za EPL ndani ya mduara wa nne-bora, Solskjaer amesisitiza kwamba itakuwa tija na fahari tele kwa mabingwa mara 20 kutoa ushindani unaostahili kwa wapinzani wao wakuu hadi mwisho wa msimu.

Katika muhula uliopita wa uhamisho wa wachezaji, Man-United walijinasia huduma za nyota watatu; Harry Maguire kutoka Leicester City, Aaron Wan-Bissaka aliyeagana na Crystal Palace na Daniel James kutoka Swansea City.

Fowadi Romelu Lukaku aliyoyomea kambini mwa Inter Milan nchini Italia.