Michezo

KAZI BADO: Tottenham Hotspur kualika Brighton huku Saints wakiendea Watford EPL

April 23rd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

TOTTENHAM Hotspur watakuwa leo Jumanne wenyeji wa Brighton katika uwanja mpya wa White Hart Lane katika mchuano wa raundi ya 35 ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Ni mechi ambayo Tottenham wana ulazima wa kusajili ushindi ili kujipa uhai wa matumaini ya kumaliza kampeni za msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora jedwalini.

Kufikia sasa, Tottenham wanaonolewa na kocha Mauricio Pochettino wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 67, moja zaidi kuliko Arsenal ambao Jumatano watapania kujinyanyua baada ya chombo chao kuyumbishwa na Crystal Palace kwa kichapo cha 3-2 ugani Emirates.

Spurs ni miongoni mwa vikosi viwili vinavyopigania nafasi ya kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Tayari Liverpool na Manchester City ambao ni mabingwa watetezi wa taji la EPL wamejipa uhakika wa kunogesha kivumbi hicho cha bara Ulaya.

Brighton kwa upande wao, Brighton watakuwa wakipania kuepuka shoka la kuwateremsha daraja mwishoni mwa kampeni za muhula huu.

Kufikia sasa, kikosi hicho kinashikilia nafasi ya 17 kwa alama 34, tatu zaidi kuliko Cardiff City ambao pia wananing’inia padogo mkiani mwa jedwali. Fulham na Huddersfield tayari wameshushwa ngazi kwenye kipute cha EPL msimu huu.

Kubwa zaidi linalotarajiwa kuwatambisha Spurs ni ubora wa rekodi yao dhidi ya Brighton.

Hadi kufikia sasa katika historia ya soka ya EPL, Spurs hawajawahi kupoteza mchuano dhidi ya Brighton.

Matokeo bora zaidi ambayo Brighton wamewahi kusajili dhidi ya Tottenham ni sare ambayo ilitokea mara moja pekee.

Nne kati ya michuano sita iliyokutanisha Tottenham na Brighton awali imemalizika kwa pande zote mbili kufungana mabao huku mechi tatu zikishuhudia zaidi ya mabao matatu yakifungwa.

Brighton wanajivunia kuwafunga Tottenham bao moja pekee kati ya mechi tatu zilizopita zilizochezewa jijini London huku wakiokota mpira wavuni mara mbili katika kila mojawapo ya michuano iliyowakutanisha ugani American Express Community.

Tottenham watashuka dimbani kwa minajili ya mchuano wa leo wakipania kuyaweka kando maruerue ya kuchapwa 1-0 na Man-City katika mechi ya awali.

Kuambulia patupu mechi saba

Kwa upande wao, Brighton watakuwa wakisaka ushindi kwa mara ya kwanza baada ya kupoteza mechi saba zilizopita.
Katika mchuano mwingine wa leo, Watford watakuwa wenyeji wa Southampton uwanjani Vicarage Road.

Jumatano itakuwa zamu ya Arsenal kuchuana na Wolves ugenini nao Manchester United wawaalike majirani Manchester City kwa dimba kali litakalotandazwa uwanjani Old Trafford.

Ushindi kwa Man-United katika mchuano huo utaweka hai matumaini yao ya kutinga mduara wa nne-bora na kufuzu kwa kipute cha UEFA muhula ujao.

Kwa upande wao, Man-City watakuwa katika ulazima wa kusaka alama tatu muhimu ili kuendeleza presha kwa viongozi wa jedwali, Liverpool.

Ratiba ya EPL (Leo Jumanne):

Watford na Southampton
Tottenham na Brighton

(Jumatano):

Wolves na Arsenal
Man-United na Man-City