Michezo

Kazi kwa Tusker, Western Stima na Vihiga KPL

April 11th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

Presha itakuwa kwa klabu za Tusker, Western Stima na Vihiga United zitakapoteremka uwanjani kumenyana na KCB, Kariobangi Sharks na Vihiga United kwenye Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mtawalia, Alhamisi.

Mabingwa mara 11 Tusker, ambao wamepata ushindi mmoja katika mechi tisa zilizopita msimu huu na hawajashinda mechi tatu mfululizo, watafukuzia ushindi wa tatu mfululizo dhidi ya KCB klabu hizi zitakapokutana uwanjani Kenyatta mjini Machakos.

Si siri kwamba vijana wa kocha Robert Matano watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya wanabenki wa KCB licha ya kuwa na rekodi nzuri dhidi yao. Mbali na kwamba nambari saba Tusker imekuwa ikitatizika kupata ushindi, inakutana na timu ya KCB ambayo imekuwa ikifanya vizuri.

Vijana wa Frank Ouna, ambao walichapwa 3-1 na Tusker mnamo Desemba 29 mwaka 2018, wamezoa ushindi mara tano katika mechi tisa zilizopita. Wanabenki hawa wanaoshikilia nafasi ya tisa, watashuka uwanjani wakitafuta kudumisha rekodi ya kutoshindwa msimu huu hadi mechi sita.

Nambari 15 Vihiga, ambayo iko alama tatu pekee nje ya mduara hatari wa kutemwa, inazuru uwanjani Sudi mjini Bungoma ikitafuta kumaliza nuksi za kulemewa na wapinzani hawa ugenini.

Vihiga ilicharazwa 2-0 ilipozuru Nzoia mwaka 2016 katika Ligi Pana na kuzidiwa maarifa 1-0 zilipokutana Septemba mwaka 2018 kwenye Ligi Kuu.

Vihiga haina ushindi katika mechi tatu zilizopita msimu huu. Nzoia ilimalizia hasira yake ya kutoshinda mechi tano kwa kukung’uta Mount Kenya United 6-1 katika mechi yake iliyopita. Wanasukari hawa, ambao wako katika nafasi ya 12, wanatumai kutumia wembe huo huo kunyoa Vihiga.

Stima imepiga sare tano na kupoteza mara tatu katika mechi zake nane zilizopita. Wanaumeme hawa wanaoshikilia nafasi ya 13 watakuwa wakilenga kulipiza kisasi dhidi ya nambari nane Sharks, ambayo iliwalima 1-0 Agosti 23 mwaka 2017 na 2-1 Januari 13 mwaka 2019 ugenini.

Stima itaalika Sharks uwanjani Moi mjini Kisumu. Zilitoka 1-1 zilipokutana mara ya mwisho katika ardhi ya Stima mnamo Mei 28 mwaka 2017.

Ratiba (Aprili 11 saa tisa alasiri):

Nzoia Sugar na Vihiga United

Tusker na KCB

Western Stima na Kariobangi Sharks

Matokeo (Aprili 10):

AFC Leopards 1-1 Kakamega Homeboyz

Chemelil Sugar 1-1 Posta Rangers

Mathare United 1-2 SoNy Sugar

Sofapaka 0-0 Ulinzi Stars