Habari Mseto

KAZI MTAANI: Elungata awaondolea hofu vijana wanaodai wazee wamechukua nafasi zao

July 16th, 2020 2 min read

Na MISHI GONGO

MSHIRIKISHI wa usalama katika eneo la Pwani Bw John Elungata amepinga madai kuwa mpango wa Kazi Mtaani umekuwa ukiajiri wazee licha ya kupangiwa kuwanufaisha vijana.

Bw Elungata alisema mfumo wanaotumia kuwasajili vijana hao ni wa kidijitali na hauruhusu mtu ambaye hayuko kwa kundi la vijana asajiliwe.

Aidha alisema kuwa wanafanya kazi kwa karibu na maafisa wa kijasusi na wale wakusajili watu ili kuhakikisha kuwa mradi huo unawafaidi vijana pekee.

“Kuna wazee wawili au watatu ambao wameandikwa kama wasimamizi lakini hawafanyi kazi. Baadhi ya watu wanaonekana wakubwa kuliko umri wao pengine kutokana na shida,” akasema Bw Elungata.

Shughuli hiyo ambayo inaingia awamu ya pili umekubwa na tuhuma za ufisadi.

Vijana kutoka maeneo mbalimbali mjini Mombasa, wamelalamika kuwa nafasi za kazi hizo zinatolewa kiubaguzi huku wengine wakisema kuwa machifu na mabalozi wanawashurutisha kulipa kitu kidogo ili kupata nafasi hizo.

Mradi huo ambao ulizinduliwa rasmi mwezi Aprili na raisi Uhuru Kenyatta, katika kaunti za Nairobi, Mombasa, Kiambu, Nakuru, Kisumu, Kwale, Kilifi and Mandera unalenga kuwapa ajira vijana katika sehemu zilizoathirika zaidi na ugonjwa was Covid-19.

Hata hivyo kwa sasa mradi huo unapangwa kutekelezwa katika kaunti zote nchini.

Mradi huo unahusisha kusafisha mitaa kwa kukata vichaka, kuzibua mitaro, kunyunyuzia kemikali za kuuwa viini, na kufagia na kusafisha barabara.

Kiongozi wa vijana katika eneo la Kadzandani eneobunge la Nyali, Wilfred Gambo, alisema tangu kuzinduliwa kwa mradi huo vijana katika eneo hilo hawajafaidika.

“Katika eneo hili tuko na vijiji takriban 30 lakini vijana waliyochaguliwa ni ww kutoka vijiji vitatu pekee,” akasema.

Bw Gambo alisema katika awamu ya kwanza ya mradi huo hakuna kijana aliyechaguliwa kutoka Kadzandani huku awamu ya pili vijana 18 pekee ndio walichaguliwa.

Alilaumu kukosa mwakilishi was serikali katika eneo hilo kuchangia kwa wao kukosa kufaidi matunda ya serikali.

Kijana mwengine Bw Omar Chai alisema hawaelewi njia zinazotumika kusajili vijana katika zoezi hilo.

Bw Chai alidai kuwa vijana waliyoletwa kusafisha eneo hilo walitoka sehemu zengine.

“Tulisikia kuwa vijana watachaguliwa kusafisha maeneo yao, lakini tunashangaa kuona kuwa vijana kutoka maeneo mengine wanaletwa hapa ilihali wazawa wa hapa tunatengwa,” akasema.

Kijana mwengine Hajj Hassan kutoka eneo la Changamwe pia alilalamika kuwa vijana wa eneo hilo hawakuhusishwa katika mradi huo.

Alisema japo waliwasilisha majina yao kwa wawakilishi wa serikali hawajapata majibu hadi leo.

“Tuko vijana wengi katika eneo hili ambao tulipeleka majina yetu lakini tunasikitika kuona kuwa hatukupewa nafasi,” akasema.

Mwingine Juma Ali kutoka eneo hilo hilo aliiomba serikali kuingilia kati kuona kuwa mpango huo unafanyika kwa uwazi bila mapendeleo.

Hata hivyo, Bw Elungata alisema kuwa shughuli hiyo inafanywa kwa uwazi na aliwasisitiza vijana kuripoti visa vya ufisadi.

Alisema katika awamu ya pili walilazimika kupunguza malipo kufuatia idadi kubwa ya vijana waliowaajiri.

“Katika awamu ya kwanza kijana alipokea Sh600 kwa siku. Hatuwezi kulipa malipo hayo kufuatia idadi kubwa ya vijana tuliowaajiri katika awamu ya pili. Tunawalipa vijana Sh450 kila siku,” akasema.

Kulingana na Bw Elungata, awamu ya kwanza ililenga vijana 18,000 huku awamu ya pili ambayo ilizinduliwa wiki iliyopita ikilenga kuajiri vijana 16,758 katika mji wa Mombasa.