Habari za Kitaifa

Kazi: Tsunami yaja

February 15th, 2024 2 min read

NA PETER MBURU

HUENDA Wakenya 300,000 wakapoteza ajira mwaka huu 2024 huku gharama ya maisha ikiendelea kupanda nazo kampuni nyingi zikipata ugumu wa kulipa mishahara.

Utafiti ulioendeshwa na Benki Kuu ya Kenya (CBK) umeashiria kuwa idadi hiyo ya Wakenya watapoteza ajira ikilinganishwa na 70,000 ambao walifutwa kazi kati ya Oktoba 2022 na Novemba 2023.

CBK iliufanya utafiti huo mwezi uliopita ikilenga kufahamu idadi ya wafanyakazi ambao watasalia na ajira 2024 ikilinganishwa na 2023.

Waajiri wengi wameashiria kuwa watawafuta kazi wafanyakazi wao kutokana na biashara kudorora wakati ambapo Shilingi ya Kenya nayo inafifia ikilinganishwa na Dola katika ubadilishanaji wa pesa.

“Waajiri katika sekta ya kibinafsi wanatarajia kutema asilimia 15 ya wafanyakazi wao. Gharama ya juu ya maisha, mazingira yasiyoridhisha ya kufanya biashara, ushuru wa juu na kupanda kwa bei ya mafuta ni kati ya changamoto zinazokabili waajiri,” ikasema utafiti huo wa CBK.

Takwimu za 2022 zilionyesha kuwa sekta ya kibinafsi imewaajiri wafanyakazi 2,077,500. Kati ya idadi hiyo, benki na sekta ya bima zimewaajiri Wakenya 70,000.

Iwapo Wakenya 2,077,500 ambao walikuwa katika ajira 2022 katika sekta ya kibinafsi kulingana na Takwimu ya Kitaifa (KNBS) watapunguzwa kwa asilimia 15, basi Wakenya 301,125 hawatakuwa na kazi mwaka 2024.

Benki zimethibitisha kuwa zitafuta angaa asilimia tatu ya wafanyakazi ziliokuwa nao 2023.

Kwa upande mwingine, wafanyabiashara nao waliashiria ‘huenda’ hawatasalia na asilimia 47 ya waajiriwa wao lakini wana uhakika watawatimua asilimia 15 ya wafanyakazi wao.

Kupotea huko kwa ajira kunatokota miezi mitatu pekee baada ya Muungano wa Waajiri Kenya (FKE) kufichua kuwa Wakenya 70,000 wamepoteza ajira tangu Oktoba 2023.

“Kila siku tunapata notisi kutoka kwa waajiri kuhusiana na nia yao ya kuwafuta wafanyakazi. Pia tunaendeleza uchunguzi kwa waajiri kufahamu athari ya gharama ya kulipa mishahara.

“Asilimia 40 ya waajiri wametuarifu kuwa wangependa kupunguza idadi ya wafanyakazi wao ili kuoana na gharama ya kuendesha biashara nchini Kenya,” ikasema FKE.

Kenya ilikuwa na wafanyakazi milioni 2.077 ya wafanyakazi mnamo 2022 ambapo 70,000 waliajiriwa benki na sekta ya bima na kuwaacha 2,007,500 katika sekta nyingine za kibinafsi.

Utafiti wa CBK umeonyesha kuwa benki huenda itatimua asilimia 19 ya wafanyakazi wake na ina hakika ya kuwafuta kazi asilimia tatu.

Kwa kuwa sekta hiyo ina wafanyakazi 70,000 kulingana na takwimu za 2022, itasalia na wafanyakazi 54,600 na ina uhakika wa kuwatema Wakenya 2,000.

Ingawa hivyo, wengi ambao walishirikishwa katika utafiti wa CBK walionyesha imani kuwa uchumi wa Kenya utaimarika ndani ya miezi 12 ijayo.

Wengi walitaja kuongezeka kwa kiwango cha uzalishaji kwenye sekta ya kilimo kutokana na mvua ambayo imekua ikishuhudiwa kama itakayochangia kushuka kwa bei ya vyakula.

Aidha, kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la kimataifa kulitajwa na wengi kama jambo litakaloipa uchumi wa nchi nafuu miezi 12 inayokuja.