Makala

Kazi ya uchoraji yamwezesha kupata hela kipindi hiki cha janga la Covid-19

July 13th, 2020 3 min read

Na SAMMY WAWERU

KIJANA Edward Gikaria ana mengi ya kujivunia katika ulingo wa sanaa, hususan uchoraji wa picha katika karatasi na kuta za majengo na pia kutia maandishi, michoro, nembo au nakshi kwenye mavazi.

Ni mwalimu mhitimu wa kiwango cha shule ya msingi.

Gikaria hata hivyo aliacha taaluma hiyo ili kufuata wito wa kipaji chake katika uchoraji.

“Niliacha ualimu kwa sababu ya mapenzi katika sanaa,” Gikaria anaeleza.

Ikiwa eneo la Mt Kenya, mtaani Githurai kiungani mwa jiji la Nairobi, karakana yake ni tajika katika masuala ya uchoraji.

Gikaria anahadithia kwamba alifuzu kozi ya ualimu 2009 na baada ya kupokezwa cheti, alifunza kwa muda wa kipindi cha miaka miwili pekee.

Anakumbuka barabara kana kwamba ilikuwa jana tu, mnamo 2011 aliipa breki taaluma ya ualimu, akazamia kupalilia na kukuza talanta yake katika sanaa ya uchoraji.

Kijana huyu pia hajasahau, wakati akiwa katika shule ya msingi alikuwa gwiji kuchora picha za viongozi wakuu serikalini, chini ya utawala wa Rais mstaafu marehemu Daniel Toroitich Arap Moi.

Anasema aliwahi kuchora picha ya Mzee Moi, na ambayo ilimvunia umaarufu shuleni.

“Nikiwa darasa la saba, pia nilichora picha ya mchezaji mstaafu wa soka Mike Okoth. Walimu wangu walifurahia jitahada zangu na kunipa motisha, huku wakiendelea kuninoa makali katika uchoraji,” Gikaria anaelezea.

Mike Okoth alikuwa mchezaji tajika wa timu ya kitaifa ya Harambee Stars na ambaye katika enzi zake alisifiwa kusakata ngozi iliyoambwa, kandanda.

Gikaria anaiambia Taifa Leo kwamba ilimgharimu mtaji wa Sh7,000 pekee kuanzisha sanaa ya uchoraji kama biashara.

Anafafanua kuwa, “Kati ya mtaji huo, Sh3,000 nilizitumia kukodi chumba ambacho kwa sasa ni karakarana yangu. Pesa zilizosalia, nilinunua malighafi, ndiyo rangi na vifaa vya kupaka na kuchora.”

Mbali na kuchora picha, wateja wengine ni wamiliki wa majengo ya biashara, shule, hospitali, na pia kutia majina au nembo kwenye mavazi.

Edward Gikaria, mchoraji, anasema ugonjwa wa Covid-19 umenogesha kazi ya uchoraji wengi wakitumia maandishi na michoro kuhamasisha vita dhidi ya ugonjwa huu. Picha/ Sammy Waweru

 

Wakati wa mahojiano, Gikaria alisema licha ya janga la Covid-19 kuhangaisha sekta ya biashara, uchoraji umenoga wengi wakitumia michoro kufanya hamasisho.

“Ninapokea oda chungu nzima hasa kutoka kwa wafanyabiashara wakitaka majengo yao yawe na maandishi ya kupigia upatu na kuimarisha soko la bidhaa,” mwanasanaa huyo akasema.

Pia, alisema wengi wamekumbatia hamasisho la vita dhidi ya virusi vya corona kwa kuandika malangoni umuhimu wa kunawa mikono kabla ya kuingia na uvaliaji maski.

“Hospitali na maduka, ndio wateja wangu wakuu wakati huu,” akadokeza.

Maduka hasa ya kijumla, yametoa maelekezo kwa wateja kwa njia ya maandishi sakafuni na pia kwenye kuta.

“Hamasisho kwa njia ya maandishi na michoro ni muhimu ili tushinde janga hili. Kama mfanyabiashara, ni busara kukumbusha wateja haja ya kujitahadharisha na kufuata mikakati iliyowekwa na wizara ya afya,” akasema mmoja wa wateja wa Gikaria, ambaye ni mmiliki wa buchari.

Sanaa ya uchoraji, imekuwa safari ambayo Gikaria ameimarika kutoka bora hadi bora zaidi. Anasema alianza kwa breshi za wino na vitambaa kama vifaa kutekeleza shughuli za uchoraji. Baadaye, aliimarika na kupata breshi za mikono, zinazotumbukizwa kwenye rangi.

Mwaka 2019 Gikaria alinunua mashine ya presha ya kupaka rangi na kuchora. Aidha, inatumia nguvu za umeme.

Zana zingine anazotumia ni pamoja na kifaa cha kuchanganya rangi na ngazi ya kusitiri mabango.

Rangi tofauti, maji, mafuta taa maalum, ni miongoni mwa malighafi katika shughuli za uchoraji.

Sanaa ni kazi inayohusisha ubunifu. Kulingana na Gikaria, bongo, macho na mikono, ndiyo humuongoza.

Anasema, huanza kwa kutazama kwa umakinifu anachopaswa kuchora. “Huibuka na mwongozo, ninachanganya rangi na kuzamia uchoraji,” anaarifu. Msanii huyu anasema uchanganyaji rangi ndiyo hatua ngumu zaidi, na inayotaji umakinifu na uangalifu.

Picha inachukua kati ya siku tatu au nne kukamilika, zingine mchoraj huyu akisema zinaenda hadi juma moja kulingana na matakwa yake.

Huduma zake zinagharimu kati ya Sh3, 000 – 50,000

“Uwekaji maandishi, nembo na pia michoro kwenye mavazi ni Sh300 kila vazi. Ingawa biashara ya nguo hivi sasa iko chini,” Gikaria anasema.