Habari

Kazungu Kambi aponea kutangazwa amefilisika

November 2nd, 2020 1 min read

Na PHILIP MUYANGA

ALIYEKUWA Waziri Kazungu Kambi amepata afueni baada ya mahakama moja kukataa ombi la kutaka atangazwe kuwa amefilisika.

Jaji Reuben Nyakundi aliamua kuwa wakili Gicharu Kimani aliyewasilisha ombi hilo ana mamlaka ya kusaka kibali cha kuuza mali ya Bw Kambi kupitia mnada au watie saini mkataba ili waziri huyo wa zamani alimlipe Sh809,595 anazomdai.

Bw Kambi ambaye sasa ni Kamishna wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC), alikuwa mteja wa wakili Gicharu katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ugavana wa Kilifi mnamo 2017.

Bw Kambi ambaye aliwania kiti hicho kwa tiketi ya Jubilee alipinga ushindi wa Gavana wa sasa Amason Kingi.

Jaji Nyakundi wa Mahakama Kuu ya Malindi ameongeza muda wa kulipwa kwa pesa hizo kwa siku 60 zaidi.

“Hatua hiyo jinsi ambavyo nimesema itatoa nafasi kwa mlalamishi (wakili Gicharu) kutaka sehemu ya mshahara wa Kambi ikatwe ili kumlipa pesa anazomdai au afuate njia zingine za kupata pesa hizo bila kutaka ombi la kutangazwa kwa Kambi kama aliyefilisika,” akasema Jaji Nyakundi.