KBF yawahakikishia Wakenya Preston Bungei atapeperusha bendera ya Kenya katika mechi za mwisho za kuingia AfroBasket

KBF yawahakikishia Wakenya Preston Bungei atapeperusha bendera ya Kenya katika mechi za mwisho za kuingia AfroBasket

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKISHO la Mpira wa Vikapu Kenya (KBF) limehakikishia Wakenya kuwa nyota Preston Bungei anayecheza nchini Denmark, atakuwepo kupeperusha bendera ya Kenya katika mechi za mwisho za kuingia Kombe la Afrika (AfroBasket) 2021 mwezi Februari.

Katika mahojiano Alhamisi, Kaimu Katibu wa KBF Ambrose Kisoi aliambia Taifa Leo kuwa utata uliozingira mzawa huyo wa Amerika na kufanya awe shabiki tu katika mechi za mkondo wa kwanza Novemba 2020 nchini Rwanda, haupo.

“Pasipoti yake ya kuonyesha ni Mkenya haikuwa tayari Morans ilipokuwa jijini Kigali. Hata hivyo, pasipoti yake sasa iko sawa. Suala hilo lilishughulikiwa mara tu mkondo wa kwanza ulipokamilika. Asiposhiriki mkondo wa pili itakuwa kwa sababu kuna sababu tofauti wala sio matatizo na paspoti yake,” alisema Kisoi.

Bungei, ambaye anaweza kucheza kama mshambuliaji ama mlinzi, atasherehekea kufikisha umri wa miaka 26 hapo Februari 23.

Alicheza mpira wa vikapu wa malipo katika klabu ya KK Jazine Arbanasi nchini Croatia na HKK Capljina nchini Bosnia & Herzegovina kabla ya kunyakuliwa na Randers Cimbria ya Denmark mwezi Desemba 2020.

Randers inashiriki Kundi A ya Ligi Kuu Denmark. Inashikilia nafasi ya pili kwa alama 20 kutokana na michuano 13. Viongozi Bakken Bears wameajiri mshambuliaji Mkenya Tylor Okari Ongwae. Bears, ambao wanashiriki Klabu Bingwa Ulaya, wanaongoza ligi kwa alama 24 baada ya kusakata mechi 13. Kundi hilo pia linajumuisha Svendborg (alama 20), Horsens na Team FOG Naestved (18 kila mmoja).

Katika mashindano ya kuingia AfroBasket 2021, Kenya Morans inakamata nafasi ya tatu na mwisho ya kufuzu. Senegal inaongoza kwa alama sita ikifuatiwa na Angola (tano), Kenya (nne) na Msumbiji (tatu). Timu hizi ziko katika Kundi B. Zitarudiana Februari 19-21 kuamua timu tatu zitakazojikatia tiketi ya kushiriki AfroBasket nchini Rwanda mwezi Agosti 2021.

You can share this post!

COVID-19: Kenya yathibitisha visa vipya 335 idadi jumla...

Polisi wachunguza kisa cha mwanamume kuzirai na kufariki...