KCB wamwaga Sh5 milioni kwenye gofu ya wanawake ya Magical Kenya Open

KCB wamwaga Sh5 milioni kwenye gofu ya wanawake ya Magical Kenya Open

Na GEOFFREY ANENE

WANABENKI wa KCB wamedhamini mashindano ya gofu ya kimataifa ya wanawake ya Magical Kenya Ladies Open kwa Sh5 milioni, Ijumaa.

Mashindano hayo ya siku nne yatafanyika katika uwanja wa mashimo 18 wa PGA Baobab katika klabu ya Vipingo Ridge, kaunti ya Kilifi kutoka Februari 2-5.

Yamevutia wanagofu 96 kutoka mataifa ya Finland, India, Uingereza, Ujerumani, Uholanzi, Kenya, Uswidi, Ubelgiji, Uhispania, Australia, Slovenia, Scotland, Italia, Ufaransa, Austria, Czech, New Zealand, Thailand, Norway, Denmark, Wales, Japan, Swaziland, Visiwa vya Amerika vya Virgin, Isle of Man, Amerika, Uswisi na Iceland.

Bingwa mtetezi ni Mjerumani Esther Henseleit.

Mkurugenzi wa mauzo na mawasiliano wa KCB, Rosalind Gichuru amesema kuwa mojawapo ya njia za kusaidia jamii ni kupitia kudhamini michezo kwa sababu kunakuza uchezaji wa wanamichezo wa kiume na kike na pia kuinua maisha yao kijamii na kiuchumi. “Mashindano ya Magical Kenya Ladies Open ni jukwaa nzuri la wanagofu wetu kutoka Kenya kushiriki mashindano ya kimataifa na kuweka taifa katika ramani ya dunia kama miamba wa michezo,” afisa huyo amesema Ijumaa.

Ameongeza, “Tunafurahia kuwa idadi ya wachezaji wa humu nchini imeongezeka mwaka huu na tunasubiri kwa hamu kubwa kuwashabikia juma lijalo.”

Kenya itawakilishwa na Naomi Wafula, Mercy Nyanchama, Nancy Wairimu, Chanelle Wangari na Jacquelyne Walters katika raundi hiyo ya kwanza ya mashindano hayo ya raundi 39 kwenye kalenda ya European Tour 2023.

Mkurugenzi wa U.COM, Dirk Glittenberg ameelezea furaha yake kwa udhamini huo kutoka KCB akisema kujitolea kwa benki hiyo kupiga michezo jeki ni kitu cha kutamaniwa.

“Ni heshima kubwa kuwa nao kama wadhamini,” amesema Glittenberg.

Mbali na Magical Kenya Ladies Open, KCB pia itasaidia msururu wa Safari Tour kwa Sh1 milioni katika duru zitakazochezewa katika klabu ya Karen Country (Februari 4-8) na Muthaiga (Februari 18-22).

Isitoshe, KCB pia imetangaza kuwa itasaidia mashindano ya gofu ya Corporate Citizens of Africa (CCA) Sustainability uwanjani Muthaiga hapo Januari 30 hadi Februari 3.

  • Tags

You can share this post!

Sitastaafu na siendi kokote, Raila asema

WANDERI KAMAU: Magoha alionyesha umuhimu wa watu kubuni na...

T L