Michezo

KCB mabingwa wa Kakamega 7s

July 21st, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa mashindano ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya mwaka 2013 na 2014 KCB wameanza makala ya 21 ya mashindano haya kwa kubeba taji la duru ya Kakamega Sevens, Jumapili.

Wanabenki wa KCB walichabanga washindi wa Kenya mwaka 2016 na 2018 Homeboyz 21-12 katika fainali ya kusisimua mjini Kakamega.

Wafalme wa Kenya mwaka 2007, 2008, 2010 na 2011 Mwamba waliridhika na nafasi ya tatu baada ya kulipua washindi wa mwaka 2015 Nakuru 24-0 katika mechi iliyoegemea upande mmoja.

Strathmore Leos, ambayo ilitemwa kutoka Ligi Kuu msimu uliopita, ilikamilisha ziara ya Kakamega kwa kulima Nondescripts (Nondies) pembamba 21-19 katika mechi ya kutafuta nambari tano.

Menengai Oilers ilinyakua taji la Challenge Trophy, ambalo ni la timu zilizoshindwa kuingia robo-fainali kuu. Oilers ilipepeta Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi, ambayo pia haitashiriki Ligi Kuu msimu ujao baada ya kutemwa pamoja na Strathmore, 17-5.

Wenyeji Western Bulls iliridhika na nafasi ya 13 baada ya kuzima Kisii 17-12 katika fainali ya nambari 13.

KCB ilimaliza makala ya kwanza ya Kakamega Sevens bila kupoteza mechi. Ilianza kampeni yake kwa kucharaza Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST) 36-10, Kisii 42-0 na mabingwa wa Kenya mwaka 2017 Kabras Sugar 29-7 katika mechi za Kundi C mnamo Julai 20.

Ilinyamazisha Strathmore 28-12 katika robo-fainali na kuchapa Mwamba 19-5 katika nusu-fainali kabla ya kurarua ‘madeejay’ wa Homeboyz ambao historia yao dhidi ya wanabenki hawa ni mbovu.

Homeboyz pia ilimaliza siku ya kwanza bila kushindwa baada ya kulima Western Bulls 27-5, Menengai Oilers 17-7 na kutoka sare 12-12 dhidi ya Impala Saracens katika Kundi A. ‘Madeejay’ hawa walichapa Nondies 15-5 katika robo-fainali, Nakuru 20-0 katika nusu-fainali kabla ya kupigwa breki na KCB.