Habari Mseto

KCB na National Bank kubuni benki yenye thamani ya Sh1 trilioni

May 20th, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kuungana kwa benki ya Kenya Commercial na National Bank kutazaa benki moja kubwa zaidi, iliyo na thamani ya Sh1 trilioni katika muda wa miaka mitatu.

KCB ina matawi Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini. Mwezi jana, ilipendekeza kununua NBK, mpango inaotarajiwa kutimia ifikiapo Oktoba mwaka huu kulingana na taarifa ya hivi karibuni kwa washikadau.

Lakini hilo litawezekana ikiwa washikadau wa benki zote na waratibu wa soko wataidhinisha pendekezo hilo.

KCB itafanya NBK moja ya tawi lake huru kwa muda wa miaka miwili baada ya kutwaa benki hiyo na baada yake kuunganisha benki hizo kuwa benki moja.

Kuunganishwa kwa benki hizo mbili kutazaa benki ya thamani ya Sh828 bilioni kuambatana na taarifa ya kifedha ya benki hizo kufikia Desemba 2018.

KCB ilikuwa na Sh714 bilioni ilhali NBK ilikuwa na Sh114 bilioni kufikia mwishoni mwa 2018.

“Ongezeko la fedha litapanua uwezo wa KCB wa kukopesha zaidi. Benki moja itabuni nafasi ya kuwa na uwezo wa Sh1 trilioni kufikia 2022,” ilisema KCB katika taarifa kwa washikadau wake.

Benki ya KCB ndiyo kubwa zaidi nchini Kenya na utwaaji huo utaifanya kubwa zaidi una kuongeza ushindani sokoni.