Michezo

KCB na Quins wapiga hatua moja mbele kwenye misimamo ya ligi ya raga nchini

February 26th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BAADA ya mechi ya mwisho ya Ligi Kuu ya raga nchini ya raundi ya 11 kushuhudia Kenya Harlequin ikidhalilisha Strathmore Leos 41-23 Jumapili, klabu za KCB, Kenya Harlequin, Impala Saracens, Nakuru na Menengai Oilers zimeruka juu nafasi moja kila mmoja kwenye jedwali.

Mabingwa watetezi KCB wamechukua usukani kutoka kwa Kabras Sugar baada ya kutitiga wanasukari hawa 44-20.

Wanabenki wa KCB wana alama 50, moja zaidi ya Kabras, ambao walikuwa wameshinda mechi 10 mfululizo kabla ya kupigwa breki.

Kabras, ambao wameteremka nafasi moja chini baada ya kichapo hicho kikali, wako alama 12 mbele ya nambari tatu Harlequin, ambao wamesukuma Nondescripts chini nafasi moja hadi nambari nne kwa tofauti ya magoli.

Nondies walilemea Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta japo kwa jasho 10-7.

Licha ya kucharazwa 29-15 na Nakuru, Mwamba wanasalia katika nafasi ya tano kwa alama 32.

Impala sasa wanashikilia nafasi ya sita kutoka saba baada ya kulima Homeboyz 36-27 na kufikisha alama 29.

Nakuru wamerukia nafasi ya saba kutoka nambari nane baada ya kushinda Strathmore.

Wana jumla ya alama 28.

Mambo mabaya kwa Homeboyz

Homeboyz ndio waliopoteza zaidi wikendi iliyopita.

Wameshuka nafasi mbili hadi nambari nane kwa alama 26.

Wanafuatiwa na washiriki wapya kabisa Menengai Oilers, ambao walijiongezea alama tano muhimu katika ushindi wao wa alama 36-15 dhidi ya Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi.

Oilers wamezoa alama 20. Blak Blad wanafunga 10-bora baada ya kuteremka chini nafasi moja. Wana alama 16.

Strathmore na Machine wanasalia katika nafasi mbili za mwisho kwa alama 10 na tano, mtawalia.

Ratiba ya mechi za raundi ya 12 (Machi 2): Menengai Oilers na KCB, Nondescripts na Homeboyz, Mwamba na Kenya Harlequin, Mean Machine na Kabras Sugar, Blak Blad na Impala Saracens, Nakuru na Strathmore Leos.