Michezo

KCB ni wafalme wa raga ya 7s, wajizolea Sh0.5 milioni

September 10th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MAKALA ya 20 ya mashindano ya raga ya kitaifa ya wachezaji saba kila upande yalikamilika Jumapili, huku KCB ikijiongezea taji la tatu kwenye kabati lake baada ya ukame wa miaka minne.

Wanabenki wa KCB walipepeta washindi wa mwaka 1999 na 2000 Impala Saracens 26-21 katika fainali kali ya duru ya mwisho ya Driftwood jijini Mombasa.

Vijana wa kocha Dennis Mwanja, ambao walitoka chini alama 14-0 wakati wa mapumziko katika mechi hiyo na kuduwaza Impala ya kocha Oscar Osir siku ya Jumapili, walikamilisha msimu kwa alama 116.

Mabingwa hawa wa Ligi Kuu ya raga ya wachezaji 15 kila upande (Kenya Cup) walipokea tuzo ya mshindi ya Sh500,000.

KCB iliingia duru ya Driftwood ikijivunia kunyakua mataji ya duru za Kakamega (Kakamega), Dala (Kisumu) na Christie (Nairobi).

Mwamba ilibeba taji la shindano lake la Kabeberi (Meru) na Prinsloo (Nakuru). Vijana hao wa kocha Kevin Wambua walitunukiwa Sh250,000 kwa kukamilisha msimu katika nafasi ya pili kwa alama 92.

Matumaini ya Mwamba kujiongezea taji la mwaka huu kwa yale ya mwaka 2007, 2008, 2010 na 2011 yalikwisha ilipofungiwa nje ya mduara wa nane-bora wa Driftwood.

Homeboyz, ambayo ilitawala mashindano haya mwaka 2018, ilijiliwaza kukamilisha msimu bega kwa bega na Mwamba kwa alama 92.

“Madeejay” wa Homeboyz waliiingia duru ya Driftwood wakiwa katika nafasi ya nne kwenye jedwali, lakini walifaulu kuruka wenyeji wa duru ya Prinsloo, Nakuru, walipomaliza katika nafasi ya nne mjini Mombasa nao Nakuru wakakosa kufika robo-fainali kuu. Nakuru ya kocha Mitch Ocholla ilifunga msimu ya nne kwa alama 90.

 

Mwanaraga wa KCB Davis Chenge akikabiliwa na mwenzake wa kikosi cha Kabras wakati wa fainali za Kenya Cup hapo awali. Picha/ Maktaba

Menengai Oilers ya kocha Gibson Weru ilikwamilia nafasi ya tano kwa alama 81.

Ilishikilia nafasi hiyo kwa pamoja na Impala.

Nondescripts almaarufu Nondies ilikamilisha mashindano haya ya duru sita kwa alama 68 katika nafasi ya sita ikifuatiwa alama 18 nyuma katika nafasi ya saba na timu ya Chuo Kikuu cha Masinde Muliro (MMUST).

Mabingwa wa mwaka 2017 Kabras Sugar, ambao walikosa Kabeberi Sevens, waliruka juu nafasi moja baada ya Driftwood na kukamilisha msimu katika nafasi ya nane kwa alama 42.

Walibadilishana nafasi ya tisa na washindi wa mwaka 2009 Strathmore Leos walioridhika na alama 38.

Nambari tatu

Washindi wa mwaka 2005, 2006 na 2012 Kenya Harlequin, ambao walianza msimu vibaya kabla ya kuimarika polepole na kumaliza nambari tatu katika Driftwood Sevens, walikusanya jumla ya alama 36.

Walisukuma Northern Suburbs Cubs nafasi moja chini hadi nambari 12 alama tatu nyuma.

Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta, Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi na Western Bulls zikamilisha msimu kwa alama 29, 18 na 11, mtawalia.