Michezo

KCB wanusia ubingwa wa raga ya 7s baada ya kufungua pengo

September 3rd, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WANABENKI wa KCB wanahitaji tu kufika nusu-fainali ya duru ya mwisho ya raga ya kitaifa ya wachezaji saba kila upande ya Driftwood, kutawazwa mabingwa wa mwaka 2019 baada ya kufungua mwanya wa alama 10 juu ya jedwali.

KCB, ambayo mara ya mwisho iliibuka bingwa wa Kenya ni mwaka wa 2014, ilinufaika pakubwa kujiweka pazuri ilipopiga wapinzani wao wa karibu Mwamba 17-12 , katika nusu-fainali na kunyakua taji la Christie Sevens uwanjani RFUEA jijini Nairobi mnamo Jumapili

Mabingwa hawa wa duru ya Kakamega na Dala, wana jumla ya alama 94 baada ya kuongeza 22 wikendi.

Washindi wa kitaifa mwaka 2007, 2008, 2010 na 2011 Mwamba wanasalia katika nafasi ya pili baada ya kufikisha alama 84. Waliambulia alama 15 uwanjani RFUEA baada ya kulemewa na Nakuru katika mechi ya kutafuta nambari tatu 21-14.

Nakuru, ambayo ilitawazwa wafalme wa Kenya mwaka 2015, iko alama moja nyuma ya Mwamba. Imeruka juu nafasi moja na kusukuma Homeboyz katika nafasi ya nne.

Mabingwa wa mwaka 2016 na 2018 Homeboyz walichapa Nondies 24-0 katika mechi ya kutafuta nambari tano na kufikisha alama 77.

Baada ya duru tano za kwanza, vita vya kuwania taji sasa vimesalia kuwa kati ya KCB, Mwamba, Nakuru na Homeboyz. Hata hivyo, KCB iko pazuri zaidi kwa sababu Mwamba na Nakuru zinategemea ikose kufika nusu-fainali nayo Homeboyz inahitaji kushinda Driftwood na pia timu hizo ambazo ziko mbele yake ziondolewe mapema mashindanoni, ili itetee taji.

Hakuna mabadiliko kutoka nafasi ya tano hadi 10 zinazoshikiliwa na Menengai Oilers (alama 71), Impala Saracens (62), Nondies (56), Masinde Muliro almaarufu MMUST (45) na Strathmore Leos (36).

Nafasi ya 11

Washindi wa mwaka 2017 Kabras Sugar wamepaa nafasi moja na kutulia katika nafasi ya 11 baada ya kujizolea alama tano katika Christie Sevens na kuwa na jumla ya alama 29.

Northern Suburbs Cubs iliyoshikilia nafasi ya 11, imeteremka chini nafasi moja. Iliambulia alama tatu wikendi. Cubs iko alama moja nyuma ya Kabras.

Washindi wa mwaka 2005, 2006 na 2012 Kenya Harlequin wamerukia nafasi ya 12 kutoka 14 baada ya kuzoa alama nane katika shindano lao la Christie Sevens.

Quins wako na alama 19 sawa na Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta iliyokwamilia nafasi ya 13 baada ya kuvuna alama saba wikendi.

Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi imeteremka chini nafasi mbili. Ina alama 15.

Western Bulls na Egerton zinafunga mduara wa timu 16-bora kwa alama 11 na tisa, mtawalia.