Michezo

KCB washinda Dala Sevens na kung’oa Mwamba kileleni

August 13th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa zamani wa raga ya wanaume ya wachezaji saba kila upande ya Kenya, KCB wamerejea juu ya jedwali na makala ya mwaka 2019 na kufungua mwanya wa alama 12 dhidi ya wapinzani wao wa karibu baada ya kutwaa taji la duru ya Dala Sevens mjini Kisumu, wikendi.

Wanabenki wa KCB wamevuna jumla ya alama 59 baada ya duru tatu za kwanza. Hawakuwa wameshinda Dala Sevens kwa miaka minne mfululizo kabla ya kurejea kwa kutwanga Menengai Oilers 30-5 uwanjani Mamboleo siku mbili zilizopita.

KCB, ambayo ilifungua msimu kwa kunyakua duru ya Kakamega Sevens na kisha kuridhika na nafasi ya nne katika Kabeberi Sevens, imeondoa Mwamba uongozini.

Mabingwa wa Kabeberi, Mwamba, ambao walimaliza Kakamega Sevens na medali ya shaba, wamesukumwa nafasi mbili chini hadi nambari tatu baada ya kushikilia nafasi ya tisa mjini Kisumu.

Wenyeji wa duru ya nne Nakuru, ambao walinyakua nafasi ya nne mjini Kakamega na Kisumu na kukamilisha katika nafasi ya tatu katika Kabeberi, wako katika nafasi ya pili kwa alama 47.

Mabingwa wa Kenya mwaka 2015 Nakuru wako sako kwa bako na washindi wa mwaka 2007, 2008, 2010 na 2011 Mwamba kwa alama 47. Oilers imeimarika kwa nafasi moja na sasa inashikilia nafasi ya nne kwa alama 46.

Imeruka wafalme wa mwaka 2016 na 2018 Homeboyz, ambao wako alama moja nyuma.

Nondies, ambayo inajivunia kushinda Ligi Kuu mara 17 na kombe la Enterprise mara 25, bado haikaribii kushinda taji lake la kwanza la raga ya wachezaji.

Inashikilia nafasi ya sita katika makala haya ya 21 kwa alama 36. Haijasonga kutoka nafasi hiyo.

Wafalme wa Kenya mwaka 1999, 2000, 2001 na 2004 Impala Saracens wameruka juu nafasi mbili na kutulia katika nafasi ya saba kwa alama 35.

Wengine washuka

Kuimarika kwao kumesukuma chini timu za Masinde Muliro (MMUST) na Strathmore Leos nafasi moja kila mmoja hadi nambari nane na tisa.

MMUST na Leos zimezoa alama 30 na 21 mtawalia. Northern Suburbs Cubs inafunga mduara wa 10-bora baada ya kupaa nafasi moja. Cubs ina alama 20.

Iko alama tano mbele ya nambari 11 Mean Machine ya Chuo Kikuu cha Nairobi iliyoshuka nafasi moja.

Baada ya kukosa Kabeberi Sevens, washindi wa mwaka 2017 Kabras Sugar walirejea katika Dala Sevens na kujizolea alama saba zilizowasaidia kuimarika kutoka nafasi ya 14 hadi nambari 12.

Wanasukari hawa wana jumla ya alama 12, mbili zaidi ya Blak Blad ya Chuo Kikuu cha Kenyatta. Western Bulls, Egerton Wasps na Kenya Harlequin zinafuatana katika nafasi za 14, 15 na 16 kwa alama nane, sita na nne, mtawalia.