Michezo

KCB yachupia kilele cha ligi baada ya sare

September 17th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

KCB imerukia juu ya jedwali la Ligi Kuu (KPL) baada ya mechi sita kati ya saba zilizosakatwa katika raundi ya pili wikendi iliyopita kumalizika bila mshindi.

Hata hivyo, KCB ilidondosha alama mbili muhimu ambazo zingeiwezesha kufungua mwanya wa alama tatu ilipokabwa na washiriki wapya kabisa Kisumu All Stars 0-0.

Wanabenki wa KCB wako sako kwa bako kwa alama nne na mabingwa wa zamani Ulinzi Stars, ambao pia waliumiza nyasi bure walipotoka 0-0 dhidi ya washindi wa mwaka 2009 Sofapaka, na Posta Rangers na Kakamega Homeboyz waliotoka 1-1.

Mabingwa watetezi Gor, ambao walikuwa kileleni baada ya mechi za raundi ya kwanza, sasa wanashikilia nafasi ya tano kwa alama tatu walizopata kwa kung’uta Tusker 5-2 Agosti 31.

Gor ya kocha Steven Pollack itapata fursa ya kuchupa kileleni tena itakapozuru Chemelil Sugar kwa mechi yake ya pili Alhamisi. Zoo FC inakamata nafasi ya sita kwa alama tatu ilizopata wiki mbili zilizopita dhidi ya Chemelil. Itaalikwa na Bandari mnamo Jumatano.

Chemelil na Zoo hazikusakata mechi zao kwa sababu Gor na Bandari zilihusika kwenye Klabu Bingwa na Kombe la Mashirikisho, mtawalia.

Kuzoa ushindi

SoNy Sugar inafunga orodha ya timu saba zilizozoa ushindi kufikia sasa.

Wanasukari hawa wana alama tatu baada ya kufuta kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa KCB kwa kuzaba Nzoia Sugar 2-1.

Western Stima, Kariobangi Sharks, Mathare United na Wazito zinafuatana kutoka nafasi ya nane hadi 11 kwa alama mbili kila mmoja. Stima na Wazito zilitoka 0-0 nazo Tusker na Mathare zikaridhika na 1-1, wikendi.

Bandari ni ya 12 kwa alama moja sawa na Nzoia, Sofapaka, AFC Leopards, Kisumu na Tusker nayo Chemelil inavuta mkia bila alama.