Habari Mseto

KCB yazoa faida ya Sh12 bilioni kwa miezi 6

August 16th, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Benki ya Kenya Commercial imetangaza ongezeko la faida la asilimia 18 baada ya ushuru katika miezi ya mwanzo ya 2018.

Alhamisi, benki hiyo ilitangaza kupata faida ya KSh12. 1 bilioni katika kipindi hicho. Akiongea wakati wa kutoa matokeo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa KCB Joshua Oigara alisema ongezeko la faida lilitokana na kuwa biashara ilikuwa imara licha ya changamoto kadhaa.

Baadhi ya changamoto zilikuwa ni mandhari mbaya ya biashara na mikopo iliyopungua katika masoko muhimu.

“Tuko shwari katika kufanikisha malengo yetu ya 2018 katika miradi sita ya kimkakati. Biashara imeendelea kuimarika hasa kutokana na hatua tulizochukua,” alisema Bw Oigara.

Kulingana na ripoti ya fedha, mapato ya jumla yaliimarika kwa asilimia tatu hadi Sh35.6 bilioni kutoka Sh34.6 bilioni.

Mapato hayo yaliimarika hasa kutokana na riba na yasiyotokana na riba.