Habari

KCPE: Siri ya kuwa juu miaka 10

November 21st, 2018 2 min read

Na DAVID MUCHUI

HUKU walimu wa shule nyingi za umma wakiandikisha matokeo ya kuaibisha kwenye mtihani wa mwaka huu wa darasa la nane (KCPE), katika shule ya Kathigiri iliyoko Kaunti ya Meru, hali ni tofauti.

Shule hii ya umma ya Kathigiri Mixed Boarding School imekuwa ikishindana vikali na zile za kibinafsi na mwaka huu imeandikisha matokeo zaidi ya kujivunia baada ya wanafunzi 54 kati ya 84 kupata alama 400 kwenda juu

Matokeo haya yamemfurahisha zaidi mwalimu mkuu Bw Eustace Micheni, ambaye anasema sasa ametimiza ndoto yake ya kustaafu kazi yake ya ualimu kwa furaha ifikapo Juni mwaka ujao.

Matokeo haya yalikuwa tu ishara ya bidii ambayo shule hiyo imekuwa ikiweka katika masomo, hatua ambayo imeifanya kuorodheshwa shule bora zaidi ya umma kitaifa katika KCPE kwa miaka 10 mfululizo.

Mwaka huu, wanafunzi shule hiyo imeandikisha alama ya wastani ya 403.7.

Matokeo haya sasa yamempa furaha isiyo kifani Bw Micheni, ambaye anatarajia kustaafu Juni mwaka ujao, akimaliza safari yake ya miaka 37 katika ualimu kwa mafanikio yasiyo kifani.

Mwaka uliopita, mwalimu huyo alituzwa tuzo ya Head of State Commendation (HSC) na Rais Uhuru Kenyatta.

“Nina furaha kuwa nitaacha sifa nzuri ya kusimamia shule bora ya umma kwa miaka 10. Ninashukuru sana wafanyikazi wenzangu kwa msaada walionipa katika kipindi hicho na natumaini mridhi wangu ataendeleza kazi hii,” mwalimu huyo aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano.

Shule hiyo ya Kathigiri, jina la Kimeru linalomaanisha sisimizi, ilianzishwa mnamo 1985 na kanisa la PCEA.

Mbali na shule yake kuwa nambari moja kati ya shule za msingi za umma kwenye KCPE, wanafunzi wake wamekuwa wakiandikisha matokeo mazuri kwenye somo la Hesabu, ambalo Bw Micheni hufunza.

Kutokana na mapenzi yake ya kufundisha, mwalimu huyo mkuu cheo cha afisa wa elimu na badala yake akaomba kukubaliwa kurudi darasani kufunza watoto wa darasa la tatu.

Alipoanza kufundisha mnamo 1982, shule yake ya Kirege katika Kaunti ya Tharaka iliibuka nambari moja eneo la Meru katika somo la Hesabu kwa miaka sita mfululizo

“Wizara ilijaribu kunipandisha cheo kutokana na matokeo niliyoandikisha katika Hesabu lakini sikutaka kwani ninapenda sana kufunza. Nilifanywa mkufunzi katika taasisi ya kushauri walimu ya Chogoria na muda mfupi baadaye nilipanda tena na kuwa mkaguzi wa ubora wa elimu,” akasema.

Baadaye alipewa cheo cha afisa mkuu wa elimu lakini akakataa: “Niliomba wizara kunirudisha darasani na mnamo 1999 nikapelekwa St Elizabeth Primary nikiwa mwalimu,” asimulia Bw Micheni.

Mwaka uliofuata alihamishwa hadi shule ya Kathigiri akiwa mwalimu mkuu na anaeleza kuwa alipotumwa huko alitangaza kuwa shule hiyo itakuwa nambari moja, lakini wengi hawakumwamini.

Lakini mwaka uliofuata alishangaza wengi shule hiyo ilipoibuka nambari moja nchini katika KCPE kwa matokeo yaliyoimarika zaidi na tangu hapo haikurudi nyuma.

Anasema kuwa siri ya mafanikio yake ni kufanya kazi kwa pamoja na walimu wenzake, bidii, kuchochea ari ya ushindi na kujenga uhusiano bora kati ya walimu na wanafunzi.

Ushauri wake kwa walimu wakuu wa shule za umma za msingi ni kuwa kikosi imara cha washikadau wa shule zao ndiyo siri ya mafanikio.