Habari

KCPE: Furaha mama wa miaka 68 kuzoa alama 143

November 21st, 2018 2 min read

Na PIUS MAUNDU

MAMA mmoja wa umri wa miaka 68 na ambaye aliacha masomo miaka 40 iliyopita, ametimiza ndoto yake ya kuendelea na elimu baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya msingi.

Bi Veronica Kaleso alishiriki Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) mwaka huu na kujizolea alama 143 katika shule ya msingi ya Unoa, Kaunti ya Makueni.

Licha ya kuwa na majukumu ya kuwalea watoto wake 10 na wajukuu wake 24, mama huyo aliwabwaga baadhi ya watahiniwa wa umri mdogo katika mtihani huo.

“Kushiriki kwangu katika mtihani huu ni hatua muhimu sana katika safari yangu ya elimu niliyokuwa nimesimamisha miaka mingi iliyopita. Nimefurahia sana matokeo yangu,”Bi Kaleso aliambia Taifa Leo akiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Nthandeni, eneobunge la Kaiti.

Katika matokeo yake, mama huyo alifaulu sana katika somo la hisabati kwa kupata alama 33, Sayansi alama 32, na Kiswahili alama 32.

Hata hivyo, alionekana kulemewa katika somo la Kiingereza ambalo alipata alama 23 na Social Studies alama 23.

Bi Kaleso ambaye alikuwa anasomea nyumbani mara nyingi alisema lengo lake la kurudi shuleni ni kusaka huduma kutoka afisi za serikali bila usaidizi wa mtu yeyote.

“Masomo pia yatanisaidia kuendesha shughuli zangu za kibiashara kwa mpangilio na kitaaluma,” alisema mama huyo ambaye ni mfugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Aliambia Taifa Leo kuwa aliachana na masomo mnamo 1969 akiwa darasa la tano kwa kukosa karo ya shule.

“Babangu alikuwa na wake wawili na alishindwa kugharimia elimu ya watoto wote.”

Baada ya kuwalea watoto wake na kuwa wa umri mkubwa, Bi Kaleso aliamua kurudi shuleni ili kutimiza ndoto yake.

Wakati wa mtihani wa KCPE, Bi Kaleso alipokea kadi 8 za heri njema kutoka kwa wajukuu wake, majirani pamoja na kina mama wenzake wa chama alipokuwa mwanachama.

Bi Kaleso anasema ana matumaini ya kujiunga na shule za sekondari haswa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutangaza kuwa wanafunzi wote waliofuzu KCPE watapata nafasi katika shule za upili.