Habari Mseto

KCPE: Kesi zaahirishwa kwa ukosefu wa polisi

November 1st, 2018 1 min read

Na TITUS OMINDE

KESI nyingi katika mahakama ya Eldoret ziliahirishwa kutokana na kukosekana maafisa wa polisi wa kutosha, ambao wanatoa ulinzi kwa mtihani wa KCPE.

Idadi kubwa ya maafisa wa polisi ambao ni wapelelezi katika kesi mbalimbali wamepewa majukumu ya kulinda na kusimamia mitihani hiyo.

Kutokana na hali hiyo kesi nyingi ambapo maafisa husika ni wachunguzi wakuu ziliahirishwa baada ya maafisa hao kukosa kufika mahakamani.

Kukosekana kwa maafisa hao kortini kumekashifiwa na wahasiriwa.

Samuel Obuya Mboya mwanafunzi wa chuo kikuu cha Eldoret ambaye anakabiliwa na mashtaka ya kupatikana na silaha kinyume cha sheria alillaamikia kuhairishwa kwa kesi yake baada ya mpepelezi kukosa kufika kortini.

“Nimekuwa nikija hapa kortini tangu Mei 19 mwaka wa 2017, kesi yangu imekuwa ikihairishwa kila mara kutokana na ukosefu wa afisa mchunguzi, hii ni kuninyima haki,” alisema mwanafunzi huyo.

Hakimu mkuu wa Eldoret Bw Charles Obulutsa alijuta kutokana na hali hiyo.

“Si kupenda kwa mahakama kuahirisha kesi, leo hii idadi kubwa ya maafisa hao wameenda kutoa ulinzi kwa mtihani wa KCPE,” alisema Bw Obulutsa

Hata hivyo hakimu huyo aliambia wananchi ambao walikuwa kortini kuwa kukosekana kwa amaafisa hao kortini kwa ajili ya mtihani si jambo geni kwani ni sera ya serikali kushirikisha maafisa wa polisi katika maswala ya usalama wa mitihani ya kitaifa.

Mbali idara ya mahakama vile vile idara ya polisi wa trafiki imeathiriwa pakubwa kutokana na ukosefu wa maafisa wa trafiki.

Idadi kubwa ya maafisa wa trafiki hawako barabarani kwani wanashiriki katika shughuli za kutoa usalama kwa mitihani.

Hatua hiyo pia imechangia kupungua kwa idadi ya kesi za trafiki kortini.