Habari Mseto

KCPE: Mayatima wachukua nambari moja katika kaunti

November 21st, 2018 1 min read

Na ABDIMALIK HAJIR

MAKAO ya watoto mayatima ya Young Muslim Children’s home mjini Garissa ndiyo yaliyoongoza kwa matokeo bora zaidi ya mtihani wa KCPE katika Kaunti ya Garissa.

Kituo hicho kinachoshughulikia watoto mayatima kutoka familia maskini, kilitoa mwanafunzi bora katika mtihani huo Kaunti ya Garissa, Mohamed Dayib aliyepata alama 429 huku wenzake 11 wakipata alama 400 na zaidi katika mtihani huo.

Dayib, aliyejawa na furaha, alisema ndoto yake ni kuwa daktari.Alisema alifaulu katika mtihani huo kwa sababu ya kutia bidii, kuwa na nidhamu na kuomba.

Mwanafunzi huyo alipongeza walimu katika kituo hicho kwa kuchangia matokeo hayo bora.“Nilitarajia kufanya vyema lakini sikutarajia kuongoza katika kaunti hii.

“Nina furaha kwamba nitajiunga na shule niliyochagua na kusomea udaktari,” aliambia Taifa Leo Dijitali.

Meneja wa kituo hicho, Mohamed Hailow, alisema Dayib alidumisha nidhamu ya hali ya juu tangu 2011 alipojiunga na kituo hicho na hata alikuwa kiranja mkuu.

Matokeo ya kijana huyu yanaonyesha kuwa hata kama mtu ni yatima au maskini, akipatiwa nafasi anaweza kufanya vyema,” alisema Bw Hailow.

Shule za kibinafsi katika kaunti hiyo zilifanya vyema ikilinganishwa na zile za umma, jambo ambalo linahusishwa na kuhama kwa walimu kufuatia kudorora kwa usalama.Walimu wengi kutoka kaunti za nje ya Kaskazini Mashariki walihamishwa 2017..