Habari Mseto

KCPE: Nairobi yaongoza kwa waliofanyia mtihani gerezani

November 18th, 2019 1 min read

Na JUMA NAMLOLA

KAUNTI za Nairobi, Kisumu na Nakuru ziliongoza kwa idadi ya wafungwa waliofanya mtihani wa KCPE mwaka huu.

Nairobi ilikuwa na wafungwa 548, ambao ni zaidi ya nusu ya wafungwa wote 1,046 walioshiriki kwenye mtihani huo wa darasa la nane.

Kwa jumla, wafungwa hao walitoka magereza katika kaunti 26 nchini. Kisumu ilikuwa na wafungwa 69, Nakuru (59), Uasin Gishu (24), Kajiado (32) na Meru 30. Wengine walitoka Kakamega (29), Trans Nzoia (28), Nyeri (24), Mombasa (22), Kericho 21 na Murang’a (19).

Kaunti za Homa Bay, Siaya, Kisii, Bungoma, Busia, Narok, Laikipia, Turkana, Makueni, Machakos, Embu, Kitui, Machakos, Kiambu, Kwale na Taita Taveta zilikuwa na chini wa yafungwa 19 kila moja.

Nazo kaunti za Trans Nzoia na Kisii ziliongoza kwa kuwa na watahiniwa wanane kila moja waliofanya mtihani huo wakiwa hospitalini. Bungoma na Migori zilikuwa na sita kila moja kati ya watahiniwa wote 112 waliofanya mtihani huo wakiwa wamelazwa kutokana na sababu mbalimbali.

Kati ya watahiniwa 2,407 waliokuwa na ulemavu, Kakamega (146), Bungoma (107) na Kiambu (103) zilikuwa na watahiniwa wengi. Nazo kaunti za Kisumu na Nairobi zilikuwa na 93 kila moja, Meru ikiwa na 92.