Habari Mseto

KCPE: Tamaduni zawazuia wazazi kusheherekea matokeo bora

November 21st, 2019 2 min read

NA WAIKWA MAINA

HUKU shamrashara za matokeo ya Mtihani wa KCPE zikiendelea kote nchini, familia za baadhi ya watahiniwa walilazimika kufika hadi makambi ambapo watoto wao wanaendelea na tamaduni ya kupashwa tohara.

Bi Esther Wanjiru ambaye alilazimika kuabiri bodaboda hadi shule ya msingi ya Ol Joro Orok ambapo mwanawe Marcus Maina aliyezoa alama 416 alikuwa akipitia mila hiyo inayoenziwa sana na jamii ya Agikuyu.

Bi Wanjiru aliwaandalia mwanawe mapochopocho na mlo mtamu kama njia ya kufurahia ufanisi wake lakini akakumbana na kizingiti alipofika kambini kwa kuwa mila na desturi ya Agikuyu haziruhusu wanawake kufika eneo la tohara.

Msimamizi wa shule ya msingi ya akademia ya Maryland, eneobunge la Ol Joro Orok, Kaunti ya Nyandarua alitaja kufurahishwa kwake na matokeo hayo kisha akapanga kuwatunuku zawadi wanafunzi watano bora ambao walipata alama 400 na zaidi.

Wawili hao walikubaliana kuwatembelea watoto hao Jumanne kwenye kambi wanakoendelea kupitia tohara chini ya uangalizi wa makini wa Muungano wa Wazee wa Jamii ya Agikuyu.

Mjini Ol Kalou, Bi Okusa Muchiri ambaye mwanawe Judah Munyaka alitia fora kwenye mtihani huo pia aliongoza ujumbe wa jamaa, marafiki na walimu lakini pia walikumbana na hali hiyo walipofika katika kanisa la Kikatoliki la Ol Kalou ila wakalazimika kushauriana na walinzi ambao walikuwa wakilinda eneo hilo linalotumiwa kama kambi kwa vijana wanaopitia tohara.

Walinzi hao walilazimika kushauriana na wazee ambao baadaye waliwaruhusu watangamane na wanao na kupiga picha pamoja na watoto wao ambao walipita mtihani huo uliotolewa siku ya Jumatatu na Waziri wa Elimu Profesa George Magoha.

Katika mila ya jamii ya Agikuyu, wanawake hawaruhusiwi kuwaona vijana watoto wanaotahiriwa na mwanamke anayeingia kwenye eneo hilo hulazimika kufanyiwa tambiko na wazee.

Wanawake kwa jamii hiyo ni watoto wadogo na ndiposa wazazi wa wavulana waliokuwa wamepita KCPE walilazimika kushauriana na wazee na kukatiza sherehe zao kwa muda walipoingia kwenye kambi za tohara.

“Mara ya kwanza sikuelewa kwa nini mama alikatazwa kumwona mwanawe ilhali yeye ndiye amekuwa akimpa malezi. Hata hivyo, nilikumbuka mambo ambayo huzingatiwa kwenye tamaduni hii,” akasema Lydia Wambui ambaye alikuwa kwenye kundi lililofika kuwapongeza wavulana waliong’aa kwenye KCPE.