Habari

KCPE: Walimu walia kutumika kama watumwa

November 21st, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

Walimu waliosahihisha mtihani wa darasa la nane mwaka huu ambao matokeo yake yalitolewa Jumatatu, wameelezea masaibu waliyopitia katika muda wa siku tano walizotumia kukamilisha shughuli hiyo.

Walisema kuwa walilazimishwa kusahihisha mtihani huo katika mazingira magumu mno yaliyosababisha vifo vya watatu miongoni mwao na kadhaa wakapata matatizo ya kiafya.

Kulingana na walimu hao ambao waliomba tusitaje majina yao kwa hofu ya kudhulumiwa, walitakiwa kukamilisha kusahihisha mtihani huo katika muda wa siku 10 lakini siku hizo zikapunguzwa hadi siku tano.

“Tulifanya kazi kama watumwa, chini ya ulinzi mkali huku kukiwa na wauguzi waliokuwa na ambulensi tayari kuhudumia wale ambao walilemewa,” alisema mwalimu mmoja.

Walimu hao walikuwa wakiamka saa kumi na moja alfajiri ili kujiandaa kuanza kazi saa kumi na mbili asubuhi.

Awali, walikuwa wakilala saa nne usiku lakini walipogundua kuwa hawangekamilisha shughuli hiyo katika muda wa siku tano ilivyohitajika, walianza kulala saa saba usiku.

“Ilikuwa kazi ya kuchoshwa ambayo iliathiri ubora wa matokeo. Ninahisi kwamba wanafunzi wetu hawakufanyiwa haki kwa sababu mazingira tuliyosahihisha mtihani huo hayakuweza kuhakikisha viwango vya juu vya ubora,” alieleza mwalimu mwingine.

Anasema idadi ya watahini ilipungua baadhi ya walimu waliosajiliwa walipojiondoa dakika ya mwisho waliposhindwa kustahimili shinikizo.

Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) lilikuwa limesajili walimu 5,795 kusahihisha zaidi ya karatasi milioni mbili za insha ya Kiswahili na Kiingereza, shughuli iliyotakiwa kuchukua siku 10.

“Hebu fikiria ilivyokuwa kwa wale tuliobaki baada ya wenzetu kusalimu amri wakiogopa presha iliyokuwepo,” alieleza mwalimu kutoka Kaunti ya Bomet aliyeshiriki shughuli hiyo.

Walimu hao walitengwa na ulimwengu kwa siku tano walizokuwa wakitekeleza shughuli hiyo. Hawakuruhusiwa kuingia katika chumba cha usahihishaji na simu zao au vifaa vyovyote vya kidijitali. Waliruhusiwa kutumia simu zao wakati wa mapumziko ambao haukuzidi dakika ishirini.

Mwalimu mmoja alikuwa akisahihisha zaidi ya karatasi 100. Kila karatasi ilikuwa ikikaguliwa na watu watatu kabla ya kuidhinishwa na kukabidhiwa maafisa wa KNEC.

“Tuliendesha zoezi hilo mfululizo. Hakukuwa na wakati wa kupumzika na kufanya makosa hakukuruhusiwa. Maafisa wa usalama walikuwa wakituzunguka. Yeyote aliyepatikana na makosa angeadhibiwa ikiwemo jina lake kuwasilishwa kwa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ili achukuliwe hatua za nidhamu,” alieleza mwalimu mwingine.

Ingawa serikali ilitaka kukamilisha zoezi hilo kwa muda mfupi iwezekanavyo ili itangaze matokeo mara moja na kuzuia visa vya udanganyifu, watahini hao walisema shinikizo ziliathiri ubora wa matokeo. Walisema kwa sababu ya uchovu hawangeweza kumakinikia kazi yao.

“Kufanya kazi kwa masaa marefu kunafanya mtu kuwa mchovu na katika hali hiyo hawezi kumakinika inavyostahili. Tungeruhusiwa kukamilisha zoezi hilo kwa siku 10 zilizokuwa zimewekwa awali, kila kitu kingekuwa sawa,” alieleza mwalimu huyo.

Afisa Mkuu Mtendaji wa KNEC, Dkt Mercy Karogo alisema wakati wa shughuli hiyo, walimu watatu, Bi Mary Litunya, Bi Gladys Musyoka na Bw Robert Muindi waliaga dunia.