Habari Mseto

KCPE: Wenye miaka mingi wafeli

November 18th, 2019 1 min read

Na LEONARD ONYANGO

WATAHINIWA wenye umri wa zaidi ya miaka 12 na watahiniwa waliokomaa wa kuanzia miaka 17 na zaidi, walifanya vibaya katika Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE).

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa jana na Waziri wa Elimu Profesa George Magoha, kati ya watahiniwa 169,937 walio na umri wa kuanzia miaka 17 na zaidi, ni 60 pekee walipata kati ya alama 401 na 500.

Kati ya watahiniwa 36,195 walio na umri wa miaka 19 na zaidi ni 11 tu walifanikiwa kupata alama kati ya 401 na 500.

Watahiniwa 19,310 walipata kati ya alama 100 na 300. Wengine 430 walipata chini ya alama 100.

Matokeo hayo pia yalionyesha kuwa kati ya watahiniwa 19,917 walio na umri wa chini ya miaka 12 ni 242 tu walifanikiwa kupata alama ya kati ya 401 na 500.

Wengi wa watahiniwa wa umri huo walipata kati ya alama 201 na 300.Idadi ya watahiniwa walio na umri wa chini ya miaka 12 iliongezeka kutoka 15,747 mwaka jana hadi 20,086 mwaka huu.

Kaunti zilizo na idadi kubwa ya wanafunzi walio na umri wa chini ya miaka 12 ni Bungoma (1,770), Bomet (1,111) na Kericho (1,144).

Kaunti zilizo na idadi kubwa ya wanafunzi walio na zaidi ya umri wa miaka 19 ni Turkana (4,013), Garissa (1,957) na Kilifi (3,716).Jumla ya wanafunzi 1,083,456, kati yao wakiwa wasichana 539,874 na wavulana 543,582, walijisajili kufanya mtihani wa KCPE wa mwaka huu.

Kulikuwa na ongezeko la watahiniwa mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana ambapo watahiniwa 1,052,344 walifanya mtihani wa KCPE.

“Jumla ya Kaunti 18 zilikuwa na idadi kubwa ya wasichana ikilinganishwa na wavulana. Kaunti hizo zinafaa kupongezwa,” akasema Prof Magoha.

Kaunti zilizokuwa na idadi kubwa ya watahiniwa wa kike ikilinganishwa na wa kiume ni Kakamega, Nairobi, Meru, Bungoma, Vihiga, Busia, Kiambu, Siaya, Kitui, Embu na Kisumu.Nyingine ni Elgeyo Marakwet, Tharaka Nithi, Kirinyaga, Nyandarua, Trans Nzoia, Mombasa na Bomet.

Idadi ya wanafunzi waliokosa kufanya mtihani hata baada ya kujisajili iliongezeka mwaka huu hadi 3,950 ikilinganishwa na watahiniwa 2,322 mwaka jana.