KCPE yaanza kwa visa vya kujifungua

KCPE yaanza kwa visa vya kujifungua

Na WAANDISHI WETU

VISA kadhaa vilishuhudiwa Jumatatu Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE), ulipoanza, huku baadhi ya watahiniwa wakilazimika kufanyia mitihani yao hospitalini baada ya kujifungua watoto na mwingine akiufanyia kwenye seli.

Wanafunzi watano katika kaunti za Nakuru, Samburu na Nyandarua walifanyia mitihani yao hospitalini baada ya kujifungua watoto Jumatatu.

Katika Kaunti ya Nakuru, wanafunzi watatu walijifungua saa chache kabla ya mtihani huo kuanza.

Mmoja wa watahiniwa hao, 15, anafanyia mtihani wake katika Hospitali ya Nakuru Level Five, baada ya kujifungua mtoto wa kiume Jumatatu asubuhi.

Mtahiniwa huyo kutoka Shule ya Msingi ya Kuresoi, iliyo katika Kaunti Ndogo ya Kuresoi Kaskazini, alikimbizwa hospitalini baada ya kuanza kulalamikia maumivu.

Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Nakuru, Bw Fredrick Osewe alisema msichana huyo alipata maumivu ya uzazi mara tu baada ya kufika shuleni.

Watahiniwa wengine ni mmoja kutoka Nakuru, aliyejifungulia katika Hospitali ya Rufaa ya Kericho na mwingine kutoka Kaunti ya Narok, aliyejifungulia katika hospitali moja mjini Nakuru.

Katika eneo la Elburgon, msichana wa miaka 17 anafanyia mtihani wake katika Kituo cha Afya cha Murinduko, Kuresoi Kaskazini baada ya kujifungua mnamo Jumapili.

Katika Kaunti ya Samburu, mtahiniwa kutoka Shule ya Msingi ya Amayian anafanyia mtihani wake katika Hospitali ya Rufaa ya Samburu.

Alipata maumivu ya kujifungua, ambapo alisaidiwa na wazazi kwa kupelekwa katika hospitali hiyo. Alijifungua kwa njia ya upasuaji. Hata hivyo, mtoto wake alifariki muda mfupi baada ya kujifungua.

Katika Kaunti ya Nyandarua, watahiniwa 11 wanafanya mtihani huo wakiwa wajawazito.

Mkurugenzi wa Elimu katika kaunti hiyo Bw Philip Wambua aliiambia Taifa Leo kwamba jumla ya watahiniwa 18 walipata mimba wakati wanafunzi walikuwa majumbani mwao kutokana na janga la virusi vya corona mwaka uliopita.

Katika kaunti iyo hiyo, mtahiniwa, 17, kutoka eneo la Njoro anafanyia mtihani wake katika seli ya polisi kwa tuhuma za kumdhulumu kimapenzi mtoto wiki moja iliyopita.

Mshukiwa huyo, aliyekamatwa wiki iliyopita, alishtakiwa kwa kumdhulumu msichana wa miaka 11 katika kijiji cha Sigotik, eneo la Nessuit, Kaunti Ndogo ya Njoro.

Alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Nakuru, Bi Eunice Kelley, ambapo aliachiliwa kwa dhamana ya Sh400,000 na mdhamini wa kiasi kama hicho au bondi Sh300,000 pesa taslimu.

Hakimu aliagiza mshukiwa aruhusiwe kufanyia mtihani wake katika Kituo cha Polisi cha Njoro.

Katika Kaunti ya Homa Bay, hali ilikuwa vivyo hivyo, baada ya watahiniwa wanne kufanyia mitihani yao hospitalini.

Wanne hao wanajumuisha wasichana watatu wajawazito na mvulana aliyeanza kuugua wiki mbili zilizopita.

Katika Kaunti ya Nairobi, Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC), Dkt Mercy Karogo, alitoa onyo kali dhidi ya wale ambao watajihusisha kwenye wizi wa mitihani.

“Hatutaki kuona visa vyovyote vya kuvunja masharti yoyote ya mitihani yaliyowekwa,” akasema Dkt Karogo.

Katika Kauti ya Mandera, Jeshi la Kenya (KDF) lilisaidia kusafirisha baadhi ya vifaa vya mitihani baada ya gari lililokuwa likivisafirisha kupata ajali.

Ripoti za Eric Matara, Waikwa Maina, Geoffrey Ondieki, Joseph Openda, John Njoroge, Faith Nyamai na Manase Otsialo

You can share this post!

Chelsea wapewa Man-City huku Leicester wakionana na...

Familia yaangamia ikimlilia Magufuli