Habari

KCPE yaanza waziri akionya wenye nia ya kufanya udanganyifu

October 29th, 2019 1 min read

Na MISHI GONGO

[email protected]

WAZIRI wa Elimu Prof George Magoha amezitaja Migori, Kisii, na Homabay kuwa baadhi tu ya kaunti ambazo kwa kiwango kikubwa ni ‘kitovu cha udanganyifu katika mtihani’ lakini akasema serikali imeweka mikakati kuzima visa vyovyote vya udanganyifu wa aina hiyo.

Ametoa onyo kali kwa watahiniwa na wadau katika sekta ya elimu dhidi ya kujiingiza kwa vishawishi vya aina hiyo.

“Ninafahamu kuna baadhi ya watu wataniona mbaya nikisema hivi, lakini ukweli ni kwamba tuna Migori, Kisii, na Homa Bay ni lazima tuziangalie kwa jicho la ndani. Sitaki kuwatia woga watahiniwa; ninachosema ni kwamba wakijaribu kujihusisha na udanganyifu tutawapata,” amesema Magoha leo Jumanne akiwa Uhuru na Kazi mjini Mombasa ambapo pia alizimulika kaunti za Mandera, na Garissa.

Alikuwa akisimamia walimu wakuu wa shule mbalimbali za kaunti ya Mombasa wakichukua vituoni karatasi za mtihani wa KCPE.

Amewataka wazazi na wadau wengine kuwapa watahiniwa mazingira mazuri ya kufanya mtihani. Amesema hakuna mtihani ambao karatasi zake zimefuja kabla ya muda wa watahiniwa kuukabili.

Wizara imeweka tayari helikopta 10 za polisi kusaidia katika usafirishaji wa karatasi za mtihani; hasa katika maeneo ambako kunashuhudiwa athari hasi za mafuriko yanayosababishwa na mvua iliyopitiliza kiwango.

“Mbali na hizo 10, pia kuna zingine 10 za kutumika katika maeneo ambako barabara zimekatika hasa Mandera, Wajir, Tana River, Marsabit, Lamu, na vilevile Kaunti ya Isiolo,” ameeleza waziri.

Amesema wamelazimika kuhamisha baadhi ya watahiniwa kutoka shule tano zilizokumbwa na mafuriko hadi vituo vinginevyo salama.

Aidha, kuhusu watahiniwa walio na mimba, Magoha ameradidi kuna ambulensi za kuwapeleka hospitalini wanaotaka kujifungua.

“Sitaki kutaja kaunti zenye idadi kubwa ya watahiniwa wajawazito, lakini hicho si kisingizio cha mwanafunzi kukosa kufanya mtihani,” amesema.