Habari Mseto

#KCPE2018Results: Usahihishaji wakamilika, matokeo kutangazwa wakati wowote

November 19th, 2018 1 min read

PSCU na Valentine Obara

MATOKEO ya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Msingi (KCPE) yako tayari kutangazwa, Rais Uhuru Kenyatta amesema.

Kulingana na rais, hapakuwa na visa vingi vya udanganyifu kwenye mtihani wa mwaka huu kutokana na ushirikiano wa wadau katika sekta ya elimu.

“Nashukuru wazazi, walimu na watahiniwa kwani visa vya udanganyifu vilikuwa vichache mno mwaka huu. Tunapongeza wote waliochangia kufanikisha usahihishaji wa mtihani huo,” akasema.

Rais Kenyatta alikuwa akizungumza Jumapili katika kijiji cha Gachororo kilicho eneobunge la Juja ambako alihudhuria ibada na kuongoza harambee ya ujenzi wa kanisa jipya la PCEA.

Alirejelea ahadi yake ya awali kwamba watahiniwa wote waliofanya KCPE watapata nafasi katika shule za upili mwaka ujao na akaomba wazazi wahakikishe wanao wanaendeleza masomo kwani serikali itagharamia karo zao.

Wakati huo huo, aliomba Wabunge wapitishe mswada wa usawa wa jinsia utakaowasilishwa bungeni wiki hii.