Habari

KCSE 2019: Raha ya ushindi

December 19th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MATOKEO ya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) ya mwaka huu yamekuwa bora kwa kiwango cha juu ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa miaka mitatu iliyopita.

Matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, yalionyesha kuna jumla ya watahiniwa 125,746 ambao wamepata alama ya C+ kwenda juu, itakayowawezesha kujiunga na vyuo vikuu.

Idadi hii imeongezeka mno ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo waliopata alama hizo walikuwa watahiniwa 90,377.

Miongoni mwao, ripoti kuhusu matokeo kutoka kwa Baraza la Mitihani ya Kitaifa (KNEC) ilionyesha, watahiniwa 627 walipata alama ya A ikilinganishwa na 315 waliopata alama hiyo mwaka uliopita. Wavulana waliopata alama ya A walikuwa 358 huku idadi ya wasichana ikiwa ni 269.

Vile vile, kuna wanafunzi 5,796 ambao walipata alama ya A-. Idadi hii imeongezeka kutoka 3,418 mwaka uliopita. Kwa waliopata A-, wavulana walikuwa wengi kwa jumla ya 3624 nao wasichana wakawa 2172.

Akitangaza matokeo hayo jana, Prof Magoha alisema ni dhihirisho kwamba kanuni kali za kulainisha usimamizi mitihani ya kitaifa sasa zimeanza kuzaa matunda, kwani matokeo yamekuwa yakizidi kuwa bora kadri na jinsi miaka inavyosonga.

Wakati mageuzi makali yalipofanywa kuhusu usimamizi wa mitihani ya kitaifa na Dkt Fred Matiang’i ambaye alisimamia Wizara ya Elimu, kulikuwa na malalamishi kutoka kwa baadhi ya wadau kwani watahiniwa wengi walifeli katika mitihani yao.

“Kutokana na jinsi matokeo ya watahiniwa yamekuwa yakizidi kuwa bora tangu tulipofanya mageuzi ya usimamizi wa mitihani, inamaanisha kwamba watahiniwa sasa wametulia na kukubali kufanya bidii kivyao wakiongozwa na walimu wao kujiandaa kwa mitihani,” akasema Prof Magoha.

Jumla ya watahiniwa 667,222 walifanya KCSE mwaka huu ambapo idadi ya wasichana na wavulana ilikaribiana. Kulikuwa na watahiniwa 355,782 wa kiume (asilimia 51.3) na 341,440 wa kike (asilimia 48.97).

Idadi ya vituo ambapo mtihani ulifanywa pia iliongezeka kutoka 10,078 mwaka uliopita hadi 10,287 mwaka huu.

“Wakati umefika sasa kwa taifa kuwa na imani katika mageuzi tunayofanyia usimamizi wa mitihani. Kuanzia kwa maandalizi, usimamizi hadi usahihishaji wa mitihani, tunatilia maanani ujuzi wa hali ya juu,” akasema waziri.

Kando na malalamishi yaliyoibuka miaka iliyopita kuhusu matokeo duni ya mitihani ya kitaifa, majuzi baadhi ya wadau wamelalamikia jinsi matokeo yanavyotolewa haraka mno.

Mwaka huu, serikali ilikuwa imeahidi kukamilisha shughuli hii kabla ya Krismasi, ambayo Prof Magoha alisema ni kwa minajili ya kuendeleza mtindo wa mageuzi ambao unalenga utendakazi bora na uadilifu katika usimamizi na usahihishaji wa mitihani ya kitaifa.

Jana, alihakikishia wadau kwamba shughuli yote inaweza kuaminika kwani waliohusika katika shughuli nzima walihakikisha kila mtahiniwa anapata matokeo yanayolingana na bidii aliyoweka.

“Sina hofu kutazama kila Mkenya machoni na kuwaambia kuwa siwezi kuongoza shughuli isiyoweza kuaminika,” akasema.

Matokeo hayo yaliyotarajiwa kutolewa saa tano asubuhi yalichelewa hadi saa tisa, baada ya waziri kukabidhi taarifa yake kwa Rais Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi.

Alikuwa ameandamana na Katibu wa Wizara Belio Kipsang, Afisa Mkuu wa Tume ya Kuwaajiri Waalimu (TSC) Nancy Macharia pamoja na Kaimu Afisa Mkuu wa Baraza Mitihani Nchini (KNEC) Mercy Karogo miongoni mwa wengine.