Bambika

KCSE: Alinur Mohamed akemewa kudai E nyingi ni sababu ya walimu

January 10th, 2024 2 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWANASIASA na mfanyabiashara Alinur Mohammed, amekemewa vikali na watumiaji wa mitandao ya kijamii kufuatia chapisho lake ambalo wengi walihisi liliwadunisha walimu.

Chapisho lake lilihusu sababu ambazo yumkini zilichangia wanafunzi 48,174 kupata alama ya E katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE 2023).

Matokeo yalitangazwa Jumatatu na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu.

Mara baada ya matokeo kutangazwa, Bw Mohamed ambaye aliwania ubunge eneo la Kamukunji kupitia tikiti ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) chini ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, alipachika posti katika ukurasa wa akaunti yake ya Facebook.

Ujumbe wake uliwashambulia walimu ambao “hupokea karo ya wanafunzi na mwishowe wanafunzi kupata alama duni”.

“Inasikitisha! Watahiniwa 48,174 walipata alama ya E katika mtihani wa KCSE 2023. Walimu wanachukua karo kutoka kwa wazazi kwa miaka minne na kuwarudishia watoto wao wakiwa na gredi ya E? Alama unayoweza kupata bila kuingia darasani au kusoma kwa kuandika tu jina lako na kuwasilisha kijitabu cha majibu,” aliandika Bw Mohamed.

Lakini wakijibu kwenye chapisho hilo, watumiaji mitandao ya kijamii kwa hasira walidai “huyu kadunisha walimu kwa kuwahusisha na matokeo mabaya”.

Meja Johnson alisema kuwa chapisho hilo kutoka kwa mwanasiasa halikufaa.

“Kuwataja walimu kwenye chapisho hilo ni kuonyesha namna ambavyo haujali,” akasema Johnson.

Naye Vincent Kirui alitaka walimu wasilaumiwe kutokana na matokeo hayo duni.

Aliongezea kuwa wakati mwingine mwalimu anaweza kutia kila juhudi lakini mwanafunzi akakosa kuwa na bidii.

“Usiwalaumu walimu tafadhali! Walimu wanatia kila juhudi lakini baadhi ya wanafunzi hawapo tayari kufanya kile wanachoelekezwa kufanya. Kwa mfano, mimi sikuwa ninafanya vizuri kwenye somo la Kemia. Mwalimu wangu alijitahidi kwa kiasi cha kujitolea kusaidia. Lakini mawazo yangu katu hayakukubaliana na Kemia… Acheni kuwalaumu walimu,” alichangia Bw Kirui.

Katika chapisho hilo, kuna wale walilaumu Baraza la Kitaifa la Mitihani Nchini (Knec) kwa kile walitaja kuwepo na dosari kwenye matokeo hao.

“Iwapo walifanya kosa kwenye matokeo ya KCPE, je, Wakenya wanaweza kuamini kwamba idadi kubwa kama hiyo ya wanafunzi walipata E?” aliuliza Lorenzo Van Ziggy.

Nchini kuna baadhi ya wanasiasa ambao inaaminika walipata alama duni japo wameimarika kimaisha.

Ni kwa mantiki hayo ambapo wengine walisema kuwa watahiniwa hao wasiwe na hofu na kwamba watafaulu tu maishani.

“Alama ya E inasimamia kufanya vyema… Watafanya vyema maishani mwao,” akadai Leah N Aluoch.

Naye Ruth Tyrannulate aliwatia moyo kwa kuandika kuwa: ” Hao watatengeneza nafasi za ajira. Hongera kwao.”