Habari Mseto

KCSE: Matokeo ya masomo 14 yaliimarika

December 22nd, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MATOKEO ya masomo 14 yaliimarika katika mtihani wa kitaifa ya kidato cha nne (KCSE) mwaka huu ikilinganishwa na masomo 13 mwaka 2017.

Na akitangaza matokeo hayo Ijumaa katika makao makuu ya Baraza la Kitaifa la Mitihani (KNEC), Nairobi Ijumaa Waziri wa Elimu Amina Mohamed alisema kuwa matokeo katika masomo 12 yalishuka mwaka huu ikilinganisha na masomo 13 mwaka wa 2017.

Katika mtihani huo, wasichana walifanya vizuri kuliko wavulana katika masomo ya; Kiingereza, Kiswahili, Dini ya Kikristo, Sayansi Kimu, Sanaa na Muundo na Somo la Uhunzi.

Nao wavulana waling’aa katika masomo mengine 20.

“Idadi ya watahiniwa waliopata gredi ya juu kabisa ya A katika KCSE mwaka huu ilipanda kutoka 142 (asilimia 0.02) mwaka wa 2017 hadi 315 (asilimia 0.05 ) mwaka huu,” akasema Bi Mohamed.

Waziri alisema idadi ya wanafunzi waliopata gredi ya kuwawezesha kujiunga na vyuo vikuu yaani C+ na zaidi ilikuwa ni 90,377 (yaani asilimia 13.77 ya watahiniwa wote) ikilinganishwa na 70,073 (asilimia 11.38) mwaka jana.

Jumla ya watahiniwa 660,204 walifanya KCSE mwaka huu, 338,628 wakiwa wavulana na 321,576 wakiwa wasichana. Idadi hii inaashiria kuwa asilimia 51.29 ya watahiniwa hao walikuwa wavulana huku asilimia 48,71 wakiwa wasichana.

“Kutokana na takwimu hizi, inaonekana wazi kuwa tunakaribia kufikia usawa wa kijinsia katika usajili wa KCSE. Tunapaswa kudumisha rekodi hiyo nzuri,” akasema Bi Mohamed.

Mtihani wa mwaka huu wa 2018 ulifanywa katika vituo 10,078 kote nchini.

Katika kaunti 18 idadi ya watahiniwa wa kike ilikuwa juu kuliko ile ya wavulana ikilinganishwa na kaunti 17 mwaka jana, 2017. Kaunti hizo ni: Taita Taveta, Kwale, Nyandarua, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Machakos, Kitui, Meru, Makueni, Tharaka Nithi, Uasin Gishu, Nandi, Laikipia, Elgeyo Marakwet, Kakamega, Vihiga na Kisumu

Jumla ya wanafunzi 1,499 wenye mahitaji maalum walifanya KCSE mwaka huu ikilinganishwa na 1,407 mwaka jana.

Kwa msingi ya umri, idadi kubwa ya watahiniwa walikuwa wa umri wa kati ya miaka 19 na 20, wakiwa na jumla ya wanafunzi 279,482 (asilimia 42.06) ya watahiniwa wote.