Habari Mseto

KCSE: Mtahiniwa aaga mara baada ya kumaliza mtihani wa hesabu

November 6th, 2018 1 min read

Na WAANDISHI WETU

MTIHANI wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) ulianza rasmi Jumatatu kwa majonzi baada ya mmoja wa watahiniwa katika Kaunti ya Nyamira kufariki muda mfupi baada ya kufanya mtihani wa kwanza wa somo la Hesabu.

Watahiniwa kadhaa nao walikabiliwa na changamoto tofauti, baadhi wakiwa wajawazito, wagonjwa, kufungwa gerezani miongoni mwa hali zingine.

Mwanafunzi aliyefariki alitambuliwa kama Keith Mong’are aliyekuwa na miaka 17 kutoka Shule ya Upili ya Gesiaga.

Kulingana na babake, Bw Joshua Ongaga, aliyeitwa shuleni baada ya tukio hilo, mwanawe alikuwa akikumbwa na matatizo ya moyo.

“Mwanangu alikuwa na matatizo ya moyo, na alikuwa akiendelea kunywa dawa hadi wakati wa kufanya mtihani wake,” akasema, kwenye kikao na wanahabari.