Habari Mseto

KCSE: Mtahiniwa afariki baada ya kugongwa tumboni

November 19th, 2018 1 min read

Na Mwandishi Wetu

MTAHINIWA wa KCSE Jumapili alifariki kutokana na kukanyagwa tumboni kimakosa na mwanafunzi mwenzake Ijumaa jioni walipokuwa wakishiriki mchezo wa soka katika uwanja wa shule baada ya kukamilisha mitihani ya siku hiyo.

Javana Onyango,17, wa shule ya upili ya mseto ya DC katika kijiji cha Randung’, kaunti ndogo ya Rangwe, alifariki akipokea matibabu katika Hospitali ya rufaa ya Homa Bay.

Naibu Kamishna wa kaunti ndogo ya Rangwe, Bw Elvis K’Olum alithibitisha mauti hayo na kusema marehemu alikimbizwa hadi hospitali ya kibinafsi ya Rodi Kopany mara tu baada ya tukio hilo kisha akahamishwa hadi hospitali ya rufaa kwa matibabu spesheli kabla ya kukumbana na mauti.

“Tulifahamishwa kuwa wanafunzi walikuwa wakicheza mpira baada ya mtihani. Kwa bahati mbaya mwenzake alimpiga teke tumboni na akaanguka chini,” alisema Bw Olum.

Mwili wa mwendazake ulihamishwa hadi chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo kufanyiwa uchunguzi zaidi.