Habari Mseto

KCSE: Mtahiniwa ajinyonga baada ya kufanya mtihani wa Bayolojia

November 16th, 2018 1 min read

Na KNA

MTAHINIWA wa shule ya upili ya wasichana ya Chebororwa katika kaunti ndogo ya Marakwet Magharibi alijinyonga kwa kutumia shuka katika bweni la shule hiyo.

Kamanda wa polisi katika kaunti ya Elgeyo Maraket Kenneth Kimani alisema kwamba walimu na wasimamizi walidhani kwamba mwanafunzi huyo alikuwa anasomea mitihani iliyosalia baada ya kufanya mtihani wa Bayolojia huku wenzake wakiendelea kufanya mtihani wa Kilimo ambaye yeye hafanyi.

Kimani alisema wanafunzi wenzake walioenda bwenini baada ya mtihani mwendo wa saa saba unusu mchana walipigwa na butwaa walipompata amejinyonga na kumwarifu mwalimu mkuu.

Kimani alisema walimkimbiza katika zahanati ya Chebororwa ambapo wahudumu wa afya walithibitisha kuwa alikuwa tayari amefariki.

Mkuu huyo alisema mwanafunzi huyo amekuwa akiugua ugonjwa wa moyo kwa muda mrefu. Aliacha kijibarua akiwashukuru wazazi wake, wanafunzi na marafiki na kusema hawezi kuendelea kuishi.