KCSE: Tana River yachechemea

KCSE: Tana River yachechemea

Na STEPHEN ODUOR

KAUNTI ya Tana River imekamilisha miaka 30 bila kuwa na mtahiniwa yeyote wa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) aliyefanikiwa kupata alama ya A.

Shule tatu ambazo zilikuwa zikiwika katika eneo hilo, ambazo ni Shule ya Upili ya Tarasaa, Shule ya Upili ya Wasichana ya Ngao na ile ya wavulana ya Hola, zimekuwa zikipata matokeo mabaya katika miaka ya hivi majuzi.

Shule za Kaunti Ndogo ambazo zilikuwa zikisifika miaka ya zamani kama vile ya wasichana ya Mau Mau Memorial na ya wavulana ya Tarasaa, ambayo ina umaarufu kwa kutoa wasomi kama vile Dkt Patrick Lumumba, zilipata alama wastani ya 3.0 na 2.7 mtawalia.

Mwalimu Mkuu wa Hola, Bw Stanley Moto, alisema kuna utovu wa nidhamu na watoto hawajajitolea kimasomo.“Wanafunzi wako tayari kupiga walimu na kupinga sheria za kusimamia shule. Kila mara huwa wanataka kwenda nyumbani bila sababu wala ruhusa,” akasema.

Kulingana naye, kuna walimu wenye tajriba ya juu katika shule hiyo ambao wana uwezo wa kufunza watoto hadi wapate matokeo bora, lakini wanafunzi wenyewe hawana ari.

Mwenyekiti wa shirikisho la wataalamu wa Tana River, Bw Imran Kofa, alisema matokeo mabaya husababishwa na ukosefu wa miundomsingi bora ya elimu na wahudumu wa kutosha wa shule hasa walimu.

Mkurugenzi wa Elimu Tana River, Bw James Nyagah, alisema jamii za eneo hilo haijajitolea kukuza desturi inayotoa kipaumbele kwa umuhimu wa elimu.“Wengi wa wazazi hawajali kuhusu elimu,” akasema.

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Serikali inakosea kuwaongezea raia maskini...

Mwaura apoteza useneta rasmi na kiti kutangazwa wazi